Waziri Mkuu Mizengo Pinda
Geofrey Nyang’oro JUMUIYA
ya Madaktari imetangaza rasmi kuanza kwa mgomo usio na kikomo kuanzia
kesho, huku ikidai Serikali imekataa kutekeleza madai yao yote
yaliyowasilishwa katika kamati ya majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.Wakati madaktari hao wakitangaza kurejea rasmi katika
mgomo huo uliositishwa miezi mitatu iliyopita, Pinda aliliambia Bunge
jana wakati akijibu Maswali ya Papo kwa Papo, kuwa mgomo huo ni batili
na haukubaliki.
Saa chache baada ya Pinda kutoa onyo hilo
lililorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio kutoka
Dodoma, madaktari hao wakiwa jijini Dares Salaam walitangaza mgomo huo
wenye lengo la kushinikiza Serikali kutekeleza madai yao.
Mgomo
huo ulitangazwa kwa waandishi wa habari na Dk Stephen Ulimboka, muda
mfupi baada ya kukamilika kwa mkutano wa ndani wa madaktari, uliofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Utamaduni la Watu wa Urusi.
Dk
Ulimboka alisema mgomo huo usio na kikomo utawahusu madaktari wa kada
zote nchini, na unatarajiwa kuanza kesho, baada ya wiki mbili walizotoa
kwa Serikali kumalizika bila ya makubaliano yoyote.
“Madaktari
kwa ujumla wao wamekubaliana kuwa watarejea katika mgomo usio na kikomo,
hii ni kutokana na kugundua kuwa hakuna dhamira ya dhati ya Serikali,
kumaliza mgogoro kati yetu na Serikali, uliodumu kwa muda mrefu sasa,”
alisema Dk Ulimboka na kuongeza,
“Serikali imetupilia mbali madai
yote yaliyofikishwa katika meza ya majadiliano baina ya wawakilishi wa
Serikali na madaktari na taarifa iliyotolewa bungeni na Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na pia majibu ya Waziri Mkuu leo,
yamepotosha kila kilichomo katika taarifa tuliyonayo sisi.”
Alifafanua
kwamba Serikali imetupilia mbali madai yote ambayo kabla ya kukubali
kurudi katika meza ya majadiliano yalionekana kuelekea kupata mwafaka.
Dk
Ulimboka alisema kuwa kauli iliyotolewa na Pinda bungeni, kwamba
walikubaliana, si ya kweli na hata posho zilizotajwa kwenye taarifa za
kamati hiyo ni za dharura kabla ya kuanza kwa vikao vya majadiliano.
Alisema
msimamo wao ni kuanzisha mgomo usio na kikomo na hakuna njia ya mkato
ya kuuzuia, njia pekee ni Serikali kurudi katika meza ya majadiliano.
Kuhusu
ushauri uliotolewa na Pinda kuwataka waende mahakamani, Dk Ulimboka
alisema jumuiya yao haiko tayari kwenda na kwamba itaendelea na
utaratibu wake wa kushinikiza madai hayo kwa njia ya mgomo.
“Sisi
hatuendi mahakamani na hakuna njia yoyote ya kuuzima mgomo zaidi ya
kurudi kwenye meza ya majadiliano yenye lengo la kufikia mwafaka wa yale
tunayotaka kukubaliana," alisisitiza.
Alisema katika madai yao
ya msingi waliyotoa serikalini, hadi sasa limetekelezwa moja tu, huku
wakishangazwa na Serikali kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti kutoka
Sh10,000 za awali hadi Sh100,000 kwa madai kuwa posho hiyo haikuwa
miongoni mwa madai yao.
“Sisi katika madai yetu hatukuliweka dai
hili la posho ya uchunguzi wa maiti, kwa sababu hilo siyo dai letu la
msingi. Kazi ya uchunguzi wa maiti siyo ya kila wakati, hufanywa tu pale
watu wanapokuwa na mashaka na kifo cha mtu husika, lakini pia haifanywi
na madaktari wote,” alisema Dk Ulimboka.
Madai ya madaktari
Katibu
wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitega alitaja madai yaliyowasilishwa katika
kamati hiyo kuwa ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini,
ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu,
posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa
kazini.
Akizungumzia dai la hali bora ya mazingira ya kazi,
alisema hadi sasa hakuna kilichotekelezwa huku hali ya utoaji huduma kwa
wagonjwa ikizidi kuwa mbaya.
“Tunaweza kusema tangu tukubali
kuingia kwenye meza ya majadiliano hali imezidi kuwa mbaya. Katika
hospitali kubwa kama Muhimbili inakosa vitendea kazi, dawa, wagonjwa
kulazwa chini huku rufaa za wagonjwa kwenda nje ikiongezeka,” alisema Dk
Chitega na kuongeza:
“Tunachotaka sisi ni huduma za afya
ziboreshwe ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya na
kupunguza rufaa za kwenda nje kutibiwa.”
Dk Chitega alitoa mfano
wa gharama zilizotumika kwa mwaka wa fedha wa 2010/11, kuwa ni Sh7
bilioni, ilhali fedha zilizotumika kwa kipindi cha mwaka huu kwa ajili
ya uendeshaji hospitali kubwa sita za hapa nchini kuwa Sh5 bilioni.
“Tulipendekeza
pia mchakato wa rufaa uboreshwe kwa kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda
nje kwa kuboresha huduma za ndani, Serikali ilianzisha Taasisi ya Mifupa
(MOI), ikapeleka madaktari kwenda kusoma India, wamekuja kufanya kazi
wamekosa vifaa wameondoka. Sisi lengo letu ni kuona fedha za nchi
zinatumika kuwasaidia Watanzania,” alisema Chitega.
Kwa upande
wake Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Godbles Charles alisema
taarifa zilizotolewa bungeni na Pinda na Dk Mwinyi zimepotoshwa na zina
lengo la kuwarejesha kwenye mgomo.
Pinda awaonya
Mjini
Dodoma, Pinda alitoa taarifa jana kwamba suala hilo liko Mahakama ya
Kazi na kuonya kwamba mgomo huo ni batili, wakati akijibu swali la
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Mbowe
alitaka kujua hatua zilizofikiwa na Serikali katika kutatua mgogoro wa
madaktari na walimu nchini, na sababu za kutotekelezwa makubaliano
yaliyofikiwa katika majadiliano.
Akijibu swali hilo, Pinda
alisema Serikali iliunda tume kushughulikia mgogoro wa madaktari ambapo
kulikuwa na madai 10 yaliyojadiliwa na kati ya hayo, madai matano
yalifikiwa mwafaka na madai mengine matano bado yanaleta mvutano.
“Ni
kweli tumekuwa na mgogoro na madaktari lakini tumekuwa tukizungumza nao
kwa kipindi chote cha tatizo hili, ili kupata mwafaka na kwa kama mwezi
mmoja tume iliyoundwa ilimaliza kazi na kuwasilisha taarifa serikalini
kwa ajili ya kufikia maamuzi,” alisema Pinda. Pia alisema Dk
Mwinyi alijitahidi kuonana na madaktari lakini haikuwezekana, ndipo
akamshauri awaandikie barua ambayo madaktari walimjibu kuwa, hawaoni
haja ya kuendelea na mazungumzo, kwani wamekuwa wakifanya kwa karibu
miezi mitatu bila mafanikio.
Waziri mkuu alisema, baada ya
Serikali kufikia hatua hiyo, ikaona ni vyema sasa irudi kwenye Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kuwa hawakuafikiana.
Alisema
kwenda CMA si mara ya kwanza, kwani awali walikwenda lakini Serikali
ikashauri ni kwa nini wasijadiliane nje na kufikia mwafaka, na baadaye
kurudi CMA ili kuandikisha makubaliano waliyofikia.
“Hivyo
tumerudi tena CMA kutoa taarifa na sasa suala hili limepelekwa
mahakamani, lakini kama Jumamosi wakianza mgomo ni kinyume cha sheria…
mimi nina wasihi sana, bado ipo nafasi ya kufikia mwafaka,” alisema
Pinda.
Alisema mambo matano ambayo wamefikia mwafaka ni kuongeza
malipo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu kwa madakari ambapo wasaidizi
sasa watalipwa Sh50,000 na madaktari Sh100,000.
Pia alisema
Serikali ilikubali kuwaondoa mawaziri na watendaji wengine wa wizara
hiyo, imeongeza malipo ya kuitwa kwa dharura na mengine kadhaa.
Waziri
Mkuu alisema mambo ambayo hawajafikia mwafaka ni pamoja na ongezeko la
mishahara ya madaktari, posho ya usafiri na nyumba na posho za kufanya
kazi katika mazingira magumu.
Mgogoro wa walimu
Kuhusu
walimu, Pinda alisema hatua iliyofikiwa hivi sasa ni nzuri kwani tayari
chombo cha majadiliano ambacho kilikuwa bado, sasa kimeundwa.
Alisema
tayari Katibu Mkuu, Utumishi, amempatia taarifa za kukamilika kwa
chombo hicho ambacho sasa kitawezesha kufikiwa makubaliano ya msingi na
hivyo kutatua matatizo ya walimu.
Waziri Mkuu, alitoa angalizo
kutokana na ujumbe wa simu unaosambazwa, ambao hata hivyo hakuufafanua,
na kuomba kusiharakishwe kufikia huko kwani baada ya muda mfupi mwafaka
wa madai ya walimu utapatikana.
Ujumbe huo ambao umesambazwa
katika mitandao ya kijamii, unasomeka: “Hebu tizama tofauti hii ya
kutisha ya viwango vya mishahara kwa watumishi wa umma wa TZ (Tanzania);
(Ajira mpya cheti) mwalimu Sh244,400, Afya Sh472,000, Kilimo/Mifugo
Sh959,400, Sheria Sh630,000. Diploma: Mwalimu Sh325,700, Afya Sh682,000, Kilimo/Mifugo Sh1,133,600, Sheria Sh871,500.
“Degree
(shahada) Mwalimu Sh469,200, Afya Sh802,200, Kilimo/Mifugo
Sh1,354,000, Sheria Sh1,166,000. Je upo tayari kuvumilia kunyanyaswa
hivyo katika utumishi wa umma wa taifa moja lenye soko la bidhaa lililo
na mfumuko wa bei wa kutisha? Ungana na CWT kudai nyongeza ya mishahara
100%, Teaching allowance (posho ya kufundisha), hardship allowance
(posho ya mazingira magumu). Wape sms hii walimu 20 tu! Mshikamano
daima.” |
No comments:
Post a Comment