Wednesday, June 6, 2012

Mbowe amkejeli Mkapa


 CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema ),kimehitimisha oparesheni yake katika mkoa wa Mtwara kwa kufanya mikutano katika kata Mbali mbali za Wilaya ya Nanyumbu,  huku Mwenyekiti wa Chama  hicho, Freeman Mbowe akimshambulia Rais Mstaafu wa awamu ya tatu , Benjeman Mkapa kwa madai ya kushindwa kutatua  kero  za  wakazi wa mkoa huo.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Makanga wilayani Nanyumbu,mkoani Mtwara,jimbo alilowahi kushika wadhifa wa ubunge kabla ya kushika wadhifa wa Urais mwaka 1995.



Alisema  inashangaza kuona eneo alikozaliwa kiongozi mkuu wa nchi,kuna kero za muda mrefu za tatizo la maji ambalo halijaweza kuondolewa na kupatia ufumbuzi wa soko la kudumu la zao la korosho hali inayowafanya wananchi wa mikoa hiyo kuendelea kubaki katika wimbi la umasikini wa kutisha.

“Mkapa amekuwa rais kwa kipindi cha miaka kumi, waziri, miaka karibu na ishirini ubalozi miaka 8 na ndiye Rais aliyehusika na ufisadi wa kutisha nchini akiuza mashirika yote ya umma,viwanda na nyumba za serikali,lakini ameshindwa kuleta maendeleo katika mikoa na hata jimbo aliloliongoza la Nanyumba” alisema Mbowe na kuongeza:

 Mbowe kuwakaba koo Membe na Ghasia
 Katika hatua nyingine Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani Bungeni amesema, atawakaba koo mawaziri wawili wa Jakaya Kikwete ambao ni Waziri wa Ushirikiano na Mambo ya Nje, Bernard Membe na Hawa Ghasia ambaye ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujibu shutuma  mbalimbali zilizoibuliwa na wananchi wa mkoa huo.

Alisema waziri wa Mambo ya Nje atalazimika kutoa majibu juu ya sera mbovu za mahusino ya kimatifa ambazo zinawafanya watanzania kunyanyaswa pindi wanavuka mipaka na kwenda nje ya nchi ile hali wageni wanaotoka nje wanathaminiwa.

Mbowe alitoa kauli hiyo kufuatia Mkazi Mmoja wa Kata hiyo, Mkapura Omary kumweleza kuwa watanzania wanaotaka kwenda nje hususani nchi jirani ya Msumbiji wananyanyasika licha ya kufuata taratibu zote za uhamiaji.


Akijibu hilo Mbowe alisema “Haya ni mtaokea ya sera mbovu za mambo ya nje,zinazokumbatia wageni na kuwanyanyasa watanzani,nitakwenda kuhoji Bungeni kuhusu hilo ili kuona namna sisi kama taifa tunavyopaswa kuchukua hatua”alisema.

Kuhusu viongozi wa serikali za mitaa wakiwamo madiwani na wenyeviti wa vijiji kutofanya mikutano na kusomea wananchi mapato na matumizi ambayo kisheria wanawajibika kufanya hivyo kila baada ya miezi mitatu alisema atamuhoji waziri wa Tamisemi.

 CCM ni janga la Taifa
Katika mkutano huo Mbowe alisema kama mradi mkubwa wa mafuta utafanikiwa na kuanza kuchimbwa chini ya utawala wa CCM, hali ya wananchi katika maeneo hayo itakuwa mbaya kuliko ilivyo sasa.

“Hivi sasa yapo mazao makubwa matatu ya biashara  ambayo kwa sasa yanapatikana Tanzania na ni katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo ni gesi, madini ya uranium na Mafuta, ikiwa mafuta tayari serikali ya CCM imeshaingia mikataba na wazungu ya kutafuta mafuta kabla hata ya kutungwa sheria ya kusimamia miradi hiyo,ikiwa bidhaa hiyo itapatikana ndani ya utawala wa CCM wananchi mtaingia katika mahangaiko makubwa ya kufukuzwa ili maeneo yenu yachukuliwa na wazungu” alisema Mbowe.                                                     habari na gazeti la mwananchi           

No comments:

Post a Comment