Wednesday, June 6, 2012

Wassira aishukia Chadema


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, amekishukia Chadema akisema nacho kina makundi yanayovutana yanayoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.

Wassira alisema makundi hayo pia yanamhusisha Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, huku akienda mbali zaidi kwamba chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeshindwa kumfukuza Mbunge wake, John Shibuda (Maswa Mashariki), ambaye alieleza wazi kuhusu makundi hayo.


Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV juzi usiku, Wassira alisema hakuna chama kisicho na makundi huku akikitolea mfano Chama cha Wananchi (CUF), kuwa kuna baadhi ya wanachama walitofautiana na kuamua kuanzisha kingine.

“Chadema nao wana makundi na ndiyo maana walitofautiana na marehemu Chacha Wangwe (aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema)… nao wana matatizo katika uongozi,” alisema Wassira na kuongeza:
“Mbowe, Zitto na hata Dk Slaa nao wana makundi ndiyo maana Zitto alipotangaza kutaka kugombea urais alionywa, tena mmoja ya waliofanya hivyo ni muasisi wa Chadema, Edwin Mtei.”

Wassira alisema hata Shibuda hivi karibuni ameibuka na kuzungumza yake, lakini chama hicho kimeshindwa kumfukuza.
Alisema ndani ya CCM kuna makundi na kwamba, matatizo yanayojadilika huku akijigamba kuwa chama kikubwa kama hicho hakiwezi kukosa matatizo.

Kuhusu siasa za majukwaani, Wassira alisema Chadema wanaeneza propaganda ili Watanzania wakiamini chama hicho kuwa kitachukua nchi mwaka 2015.
“Haya ni majigambo tu, mimi ni mzoefu na nimeanza siasa tangu utotoni, hizi ni siasa ambazo unaweza kuzifananisha na uganga wa kienyeji,” alisema Wassira.

No comments:

Post a Comment