DAKTARI
kutoka Hospitali Taifa Muhimbili ameieleza Mahakama Kuu Dar es Salaam
kuwa kifo cha Swetu Fundikira kilisababishwa na damu kuganda kwenye
ubongo baada ya kugongwa na kujeruhiwa kichwani.
Daktari huyo,
Paul Mwalali (48) alieleza hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika
kesi ya mauaji ya Fundikira aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Januari
24, 2010 inayosikilizwa na Jaji Zainabu Muruke.
Ilidaiwa na upande
wa mashtaka katika kesi hiyo kuwa Fundikira alifariki dunia baada ya
kupigwa na kuumizwa na askari watatu, wawili kati yao wakiwa ni askari
wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na askari mmoja wa Jeshi la Wananchi
(JWTZ).
Washtakiwa hao ni MT 1900 Sajenti Roda Robert (42) wa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni, MT 75854 Koplo Ally
Ngumbe (37) wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067
Koplo Mohamed Rashid wa JKT Mbweni.
Washtakiwa hao wote kwa
pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo la kumuua Fundikira kwa makusudi
Januari 23, mwaka 2010 saa 7:30 usiku Wilaya ya Kinondoni katika
barabara ya Mwijuma.
Katika ushahidi wake mahamakani akiongozwa na
Wakili wa Serikali Charles Ishengoma, alidai kuwa katika uchunguzi
wake alibaini kuwa kichwa cha marehemu kilikuwa na majeraha na kwamba
baada ya kukipasua ndani aliona damu imeganda karibu na fuvu.
Hata
hivyo shahidi huyo ambaye ni mtaalam wa Kitengo cha Uchunguzi wa
Mazingira na Chanzo cha vifo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
alidai kuwa fuvu lake lilikuwa salama pamoja na sehemu mbalimbali za
mwili.
Aliendelea kudai kuwa Januari 26, mwaka 2010 alikabidhiwa
taarifa ya Polisi (PF 99) ikimtaka kufanya uchunguzi wa chanzo na
mazingira ya kifo cha Swetu Ramadhani Fundikira.
“Nilipoanza uchunguzi
nilibaini kuwa mwili wa Fundikira ulikuwa na majeraha kichwani.
Niliendelea
kufungua kichwa chake karibu na fuvu kulikuwa na damu iliyoganda sehemu
iliyo karibu na uti wa mgongo. Nilichunguza fuvu lakini halikuwa na
mpasuko wowote,” alidai Dk Mwalali.
Dk Mwalali aliongeza kudai kuwa
katika uchunguzi wake walibaini kuwa ni kichwani tu ndiko kulikuwa na
matizo lakini sehemu nyingine za mwili zilikuwa salama.
“Kwa
ujumla kifo cha marehemukilisababishwa na kuumia baada ya kichwa
kugongeshwa na msukumo mkubwa uliosababisha damu kuchanganyika na ubongo
na kuganda,” alisisitiza.
Kwa upande wake, shahidi wa tano, Koplo
Eustus katika ushahidi wake alidai kuwa siku ya tukio walimkuta
Fundikira akiwa amelala chini akiwa mtupu kama alivyozaliwa, huku
akitokwa na damu mdomoni.
Koplo Eustus alidai kuwa mshtakiwa wa
kwanza na wa tatu walikuwa wamesimama pembeni yake huku wakitoa lugha za
matusi na kwamba walipowahoji kuna tatizo gani wakawajibu kuwa ni
askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Aliendelea kudai kuwa
alipowauliza kuwa mbona huyo mtu yuko mtupu kama alivyozaliwa kuna
tatizo gani, walinijibu kuwa amevua nguo mwenyewe na kwamba ameziacha
kwenye gari.
“Lakini hali ya yule mtu ilikuwa mbaya sana
ikabidi tuwaweke chini ya ulinzi na kuwafikisha katika kituo cha polisi
Selander Bridge,” alidai shahidi huyo.
Koplo Eustus amba ni askari
mpelelezi kutoka Mkoa wa Kipolisi Ilala aliendelea kudai kuwa
alipowahoji sana mshtakiwa wa kwanza alijibu kuwa Fundikira alijirusha
mwenyewe kutoka kwenye gari yao.
Alidai kuwa alishangazwa sana na
majibu yao kwa kuwa anavyofahamu askari hawezi kumuweka mtuhumiwa
pembeni badala yake ni lazima akae katikati ili kulinda usalama wake.
“Washtakiwa walifanya makusudi kumvua nguo na kumdhuru Fundikira,” alisisitiza shahidi huyo. Kesi
hiyo itaendelea kusikilizwa leo mahakamani hapo ambapo mashahidi zaidi
wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi wao.
Mapema mahakamani
hapo jana washtakiwa walisomewa shtaka lao kuwa , Januari 23, 2010 saa
7:30 usiku Kinondoni katika barabara ya Mwijuma, wanadaiwa kumuua
Fundikira kwa makusudi.
|
No comments:
Post a Comment