Wednesday, June 6, 2012

MCT yawaangukia wahariri wa habari

BARAZA la Habari nchini ( MCT ) limewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kushirikiana kikamilifu na MCT ikiwa ni pamoja na kutoa maoni mbalimbali badala ya kujitenga kama ilivyo sasa.

Katibu Mkuu wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema hayo jana  alipozungumza katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa mashauriano baina ya wahariri na MCT uliofanyika mjini Morogoro ambao unaojadili kuimarisha weledi na uwajibikaji wa taaluma ya habari nchini.


Alisema wahariri ni miongoni mwa wanachama wa MCT kupitia vyombo vyao vya habari ambapo alisema kuwa kinachoshangaza ni kuona wahariri hao wanajitenga na baraza hata katika kusukuma ajenda mbalimbali na hivyo kuviachia vyama vya waandishi wa habari wa mikoani kuwa na nguvu ya kusukuma ajenda zao.

“Wahariri ni wenye uwezo mkubwa wa kufanya uamuzi mbalimbali katika vyombo vyao ikiwamo kuruhusu habari ziingie na kutoka na hivyo wana uelewa na ndio wanaoowaongoza waandishi wao hivyo wao ndio walitakiwa kuwa na nguvu kubwa ya kusukuma ajenda za MCT,” alisema.

Aidha aliwasisitiza wahariri hao kuchukua nafasi zao kama wanachama wa MCT katika kutoa maoni na ili itende kwa matakwa vyombo vya habari wanavyotoka.

Alisema kuwa MCL imekuwa ikifanya shughuli zake za kusuluhisha migogoro mbalimbali ikiwamo ya wahariri na waandishi wa habari na hata wadau na waandishi au vyombo vya habari na wanachama wamekuwa wakinufaika kupitia usuluhishi huo badala ya watu kukimbilia mahakamani ambako mara nyingi huishia pabaya.

Hata hivyo alisema kuwa kamati ya maadili ya MCT imekuwa ikitekeleza shughuli zake kwa asilimia 90 hali ambayo ni ya kujivunia katika tasnia ya habari na hivyo wahariri wamekuwa wakikubaliana na uamuzi wa MCT.

No comments:

Post a Comment