BAADA
ya kusafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amebaini hujuma nzito katika Shirika la
Reli Tanzania (TRL) ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi
viwango vya nauli na ameagiza afukuzwe kazi.
Licha ya kuagiza
kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa
kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa
malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka
10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.
Juzi,
Dk Mwakyembe ambaye tayari amewang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), aliamua kusafiri kwa treni hadi Dodoma akitokea Dar es
Salaam ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo.
Mara baada ya
kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, Waziri Mwakyembe
alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo,
amepata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria.
Dk
Mwayembe alisema ingawa safari ilikuwa nzuri, kuna mengi ambayo
ameyabaini ambayo ni pamoja na abiria kulipa nauli kubwa na kuandikiwa
tiketi tofauti jambo ambalo alisema ni wizi na kamwe wizara yake haiwezi
kulifumbia macho.
“Unakuta nauli halali ni Sh9,000 lakini,
abiria ameandikiwa Sh29,000. Sasa nimeagiza huyu anayehusika afuatiliwe
na kujulikana na nipewe taarifa ameondolewa,” aliagiza Dk Mwakyembe.
Alisema
pia katika safari hiyo, alibaini uchakavu mkubwa wa mabehewa na hakuna
tofauti ya daraja la tatu na la kwanza, upungufu mwingine ni katika
utendaji na taratibu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa hatua.
Dk
Mwakyembe alisema si vyema mtoto kuanzia miaka mitatu kulipishwa nusu
nauli, kwani taratibu zinapaswa kufanywa ili hadi mtoto wa miaka 10
ikiwezekana asilipishwe nauli kwani treni ndiyo usafiri wa umma.
Kuhusu
mizigo, alisema kwa sasa mizigo ya abiria inalipiwa kwa kilo kama
ilivyo usafiri wa ndege jambo ambalo si sawa kwani mzigo wa abiria
kuanzia kilo 20 unalipishwa jambo ambalo linapaswa kuangaliwa.
“Usafiri
huu mimi nasema ndiyo wa umma hivyo, tusizuie watu kupeleka hata zawadi
nyumbani kwao ni vyema tuwe na utaratibu walau mizigo kidogo ya abiria
isilipiwe,” alisema Dk Mwakyembe.
Safari tatu kwa wiki
Akizungumzia
tatizo la ratiba za usafiri, Dk Mwakyembe alisema mipango inafanywa ili
kufikia Desemba, mwaka huu walau kuwe na safari tatu za kutoka Dar es
Salaam hadi Kigoma na Tabora na kuondoa kero zilizopo sasa.
Waziri
huyo alisema anaamini safari hizo zikirejea, zitapunguza wingi wa
abiria na msongamano wa watu kwenye treni na pia zitasaidia kuanza kwa
usafirishaji wa mizigo kwa kutumia usafiri huo.
“Tutawaomba wabunge
wapitishe bajeti yetu na wapande treni ili kuona usafiri huu, nina amani
tukiondoa upungufu kidogo, huu utakuwa usafiri mzuri sana,” alisema.
Hujuma
Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba ambaye allimpokea Dk Mwakyembe
alisema licha ya kuwepo hujuma katika nauli za abiria, pia wamebaini
hujuma kubwa katika mizigo inayosafirishwa kwa reli katika mashirika
yote ya TRC na Shirika la Tanzania na Zambia (Tazara).
Alisema
maofisa wasio waadilifu wa mashirika hayo, wamekuwa wakisafirisha mizigo
mingi lakini inayoandikiwa na kulipwa serikalini ni ile yenye uzito
mdogo.
“Utakuta mzigo wa tani 40 hadi 60 unaandikiwa tani 10 au
20 fedha nyingine zinaingia mifukoni mwa wajanja, hatutakubali jambo
hili,” alisema Dk Tzeba
Alisema yeye na waziri wake, pamoja na
maofisa wengine, watakuwa wakisafiri kwa kushtukiza kwa reli mara kwa
mara ili kubaini hujuma zote na kuwachukulia hatua wahusika mara moja.
“Mimi
nilikuja hapa Dodoma kwa kiberenge na baadhi ya wabunge wa kamati ya
miundombinu na leo amekuja waziri kwa treni hii haitakuwa mara yetu ya
kwanza, tutasafiri sana kwa reli ili kubaini hujuma zilizopo,” alisema
Dk Tzeba. |
|
No comments:
Post a Comment