Thursday, June 14, 2012

Makachero wamhoji mshukiwa ugaidi

MAKACHERO wa Polisi nchini wakishirikiana na wenzao kutoka nchi tatu za kigeni ikiwamo Ujerumani, wanamhoji  Emrah Edogan (24), raia wa Ujerumani anayetuhumiwa kuwa mwanachama wa kundi la Kigaidi la Al-Qaeda.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia anajulikana kwa jina la Abdulrahaman Othuman, ni raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki anatajwa kuhusika na matukio ya kigaidi yaliyotokea katika nchi za Afghanistan na Somalia.

Edogan alikamatwa jijini Dares Salaam na Makachero wa Polisi wa Tanzania mnamo June 10, katika kipindi ambacho nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki ikiwamo Kenya na Uganda, zikiwa tayari zimekumbwa na matukio ya kigaidi yanayofanywa na  Kundi la Al-Shabab la  Somalia, ambalo liinatajwa kuwa tawi la Alqaeda.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam jana, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) Robert Manumba, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Issaya Mngulu alisema Edogan anatajwa kushiriki mapambano ya kigaidi yanayodaiwa  kuratibiwa na Mtandao wa Al-Qaeda nchini Afghanistan.

Mngulu alimtaja pia mtuhumiwa huyo kuwa  anatajwa kuhusika na matukio mengine ya  kigaidi ya hivi karibuni yaliyotokea nchini Somalia, ambako alikuwa akishirikiana na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab.

“Mtuhumiwa huyu ni mpiganaji wa Al-Aqaeda ambaye ameshiriki mapambano nchini Afghanstan pia ya  hivi karibuni nchini Somalia ambako alikuwa akishirikiana na kikundi cha  kigaidi cha Al-Shabab,”alisisitiza Mngulu.

Mngulu alifafanua kwamba,  kwa sasa makachero wa hapa nchini wanafanya mahojiano na  mtuhumiwa huyo wakishirikiana na wenzao kutoka nchi za kigeni za Ujerumani, Uganda na Kenya.

Alitaja sababu za kushirikisha nchi za Kenya na Uganda ni kutokana na matukio ya kigaidi yaliyotokea katika nchi hizo yakihusisha kikundi cha Al-Shabab na kwa Ujerumani,  inahusishwa kutokana na mtu huyo kuwa raia wa nchi hiyo.

Nchini Uganda watu 70  walilipotiwa kuuwa kutokana na mlipuko wa bomu katika shambulio lililodaiwa kutekelezwa  na kundi la Al-Shabab huku wengine wengi kati yao wakijeruhiwa vibaya, wakati wakiangalia Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.

Tukio la kigaidi pia lilitokea nchini Kenya Mei 28 mwaka huu, likihusisha   mlipuko uliotokea katika jengo la Assanad Mjini Nairobi  ambako watu zaidi ya 23 walijeruhiwa vibaya.

Katika Mkutano huo wa jana, Mngulu alisema,“Hivi karibuni yalitokea matukio ya kigaidi katika nchi za Kenya na Uganda. Hivyo, tumeona kwa kuwa tuhuma zinazomkabili mtuhumiwa ni za  kigaidi, wenzetu kutoka katika nchi hizo wanaweza kuwa na taarifa zaidi juu ya uhusika wake,”alisema Mngulu.

Mngulu alipongeza wananchi kwa kuonyesha ushirikiano mzuri na vyombo vya usalama katika kufaniksiha kazi hiyo aliyodai ushirikiano wao na vyombo vya ulinzi ndio uliowezesha kufanikisha kukamatwa kwake.

“Vyombo vya ulinzi na usalama viko imara kukabiliana na matukio yoyote ya uhalifu, yakiwamo ya kigaidi, tunazidi kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo hivyo ili kuimarisha hali ya amani, usalama na utulivu hapa nchini,”alisema Mngulu.

Mabomu ya 1998
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo nchini ambaye aliwahi kuishi katika mji wa Waziristan nchini Afghanistan mwaka 2010, kumekuja wakati bado majeraha ya mlipuko wa mabomu yaliyofanywa na Alqaeda katika Ubalozi wa Marekani nchini, yakiwa bado hayajasahaulika.

Katika mlipuko huo wa mabomu uliotokea kwa wakati  mmoja na mlipuko mwingine katika ubalozi wa Marekani Nairobi, inadaiwa aliyekuwa kiongozi wa Alqaeda Osama Bin Laden alitumia dola 50milioni (zaidi ya Sh50 bilioni) kulipua Ubalozi wa Taifa hilo kubwa na tayari Mtanzania Ahmed Ghailan anashikiliwa gerezani nchini Marekani.



No comments:

Post a Comment