Tuesday, February 11, 2014

SERIKALI MBILI SI SERA YA CCM-SUMAYE


Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye

Na Baltazar Mashaka,MWANZA

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,amesema serikali mbili,si sera wala msimamo wa CCM, ingawa binafsi anapendekeza Muundo wa Serikali mbili badala ya tatu kama ilivyo kwenye mapendekezo ya mabadiliko ya Rasimu ya Katiba.

Sumaye Waziri Mkuu  wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema wanaodai kuwa Sera ya CCM ni serikali mbili wanakosea.Hata vyama vya upinzani  pia vinakosea vinapodai  msimamo wao ni serikali tatu .

Sumaye alitoa kauli hiyo Jijini Mwanza leo, wakati akihojiwa na Waandishi  wa habari waliotaka kufahamu nini maoni yake kuhusu kipengele cha muundo wa serikali tatu,kiinachodaiwa kuwa msimamo wa CCM ni serikali mbili .

Alisema jambo la msingi ni kutilia maanani kauli ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa,twende kujadili Katiba mpya kwa maslahi ya Watanzania,badala ya vyama vyetu.

“Nadhani  watu wanachanganya,suala si msimamo wala sera ya CCM kutaka muundo wa serikali mbili.Hapana, wanakosea, ingekuwa sera ya chama,basi hata mabadiliko hayo ya kuandika katiba mpya yasingefanyika.Wapinzani nao wamepita wakisema msimamo ni serikali tatu,”alisema

Katika  kuonesha kuwa hafurahishwi wala kupendezwa na kipengele hicho, alisema haiwezekani kuwa na Viongozi  Wakuu wa nchi watatu ambao kila mmoja atakuwa akipigwa mizinga 21.

Alieleza kuwa wapo watu wanaosema mfumo wa Muungano wetu hauko sahihi, wakidai mambo mengi hayajatatuliwa, hivyo suluhu yake ni serikali tatu, wanakosea na haipendezi kuwa na marais watatu katika nchi moja.

“ Kwa hili lazima tuangalie,kuwa na serikali tatu ni kuvunja Muungano .Na ukiangali kwenye rasimu hiyo, Zanzibar  wao wanasema hawako  tayari kuchangia uendeshaji wa serikali tatu.Sasa  jiulize wewe Mtanganyika utakuwa tayari kodi unayolipa kuhudumie wewe,ikupe maji,barabara,huduma za afya  na kusomesha mwanao ikaendeshe nchi nyingine ?” alihoji

Alidai binafsi wakati bado tukifikiria  ni jinsi  gani tutaingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni vema tukatafakari na kuendelea na mfumo wa serikali mbili.

Sumaye alisema Zanzibar wanadai ni nchi ndogo, hivyo hawako tayari kugharamia uendeshaji wa  serikali Muungano,hivyo iendeshwe kwa rasilimali za Tanganyika,jambo ambalo alidai halitawezekana na kung’angania serikali tatu,ipo hatari ya muungano kuvunjika.

Kuhusu kuwania Urais baada ya Rais JK kumaliza muda wake, alisema muda ukifika kama atakuwa na nia hiyo atatangaza,lakini kwa sasa  ni mapema mno kwake.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema ili nchi iendele inahitaji kuwa na uchumi imara endelevu na viwanda endelevu vinavyozalisha bidhaa zenye ubora wa kushindana kwenye soko.

Alisema serikali maskini haiwezi za kutoa huduma bora na muhimu kwa wananchi,hivyo wataendelea kuwa maskini, hali inayosababisha kuwepo kwa rushwa na upendeleo wa kutoa huduma.

Aidha alionya kuwa elimu inayotolewa nchini kwa sasa si bora inayolenga kumsaidia mtoto kujiajiri baada ya kuhitimu masomo,hali ambayo alidai inazalisha mabataka ya walio nacho na wasio nacho.

No comments:

Post a Comment