WATOTO
wenye umri chini ya miaka 18 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali au
waliohukumiwa huwekwa sehemu moja na watu wazima katika Gereza la
Segerea, Dar es Salaam na baadhi yao kuingiliwa kinyume na maumbile na
kuharibiwa vibaya.
Tuhuma hizo nzito dhidi ya magereza
zilibainika wakati Kamati ndogo ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, ilipokuwa
ikiwasilisha kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa
na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kile ilichokiona katika
gereza hilo baada ya kufanya ziara.
Kamati hiyo ilitoa taarifa
yake katika kikao kilichofanyika Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam
wiki iliyopita ambacho pia kilihudhuriwa na maofisa mbalimbali wa Jeshi
la Magereza akiwemo Kamishna wake Mkuu, Augustino Nanyaro.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Kamati hiyo ya Ukimwi
ilieleza kwamba watoto chini ya miaka 18 wanaofika katika gereza hilo
kwa makosa mbalimbali, utambulisho wao huonyesha kuwa wana miaka 19 hadi
20.
Taarifa hizo zilidai kwamba watoto hao ambao hukaa na
wakubwa mchana, usiku huhamishiwa sehemu nyingine na kuingiliwa kinyume
na maumbile kutokana na mazingira yalivyo ya kukosa pa kukimbilia.“Waligundua
mengi sana, walisema kuwa watoto hao wengi wameharibika sehemu zao za
siri. Kutokana na hali hiyo wanaowafanyia vitendo hivyo huwatumia pia
kuingiza simu, sigara, bangi na dawa za kulevya gerezani. Wanaingiza
vitu hivyo kwa kutumia sehemu zao za siri zilizoharibiwa,” kilisema
chanzo cha habari kutoka kamati hiyo na kuongeza:
“Unajua huwa
wameharibika kwa hiyo sehemu zao huwa wazi na kubwa kiasi kwamba ni
rahisi kuficha simu, bangi, sigara na dawa za kulevya bila kujulikana.”
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rosweeter Kasikila alipoulizwa jana kuhusu
tuhuma hizo alisema katika kikao hicho walipendekeza wakubwa kutengwa na
watoto na kushauri upelelezi wa kesi kufanywa mapema ili kupunguza
msongamano wa watuhumiwa.
“Hali siyo nzuri yaani sehemu ya
kuwekwa watu 40 wanawekwa watu 180. Jambo ambalo hatukulipenda ni jinsi
watoto walivyokuwa wakiwekwa sehemu moja na watu wazima kwa sababu
hujifunza mambo mengi ambayo si mazuri kwa umri wao” alisema Kasikila.
Alisema
kitendo cha watoto kukaa sehemu moja na watu wazima ndicho
kinachosababisha hata kufanyiwa vitendo vichafu ikiwa ni pamoja na
kuingiliwa kinyume na maumbile.“Tulieleza wazi kwamba watoto wanatakiwa
kutengewa sehemu yao kwa sababu wakiwa wao wenyewe si rahisi kufanyiwa
vitendo hivyo,” alisema Kasikila.
Kwa mujibu wa chanzo chetu,
katika kikao hicho maofisa wa magereza walipoulizwa kuhusu umri wa
watoto hao walisema jambo hilo lipo ila hushindwa kufanya lolote kwa
kuwa vielelezo vinavyoletwa huonyesha kuwa umri wao umezidi miaka 18.
Habari zaidi zilieleza kwamba maofisa hao walisema hali hiyo inatokana na mfumo uliopo na kwamba unatakiwa kufanyiwa kazi.
Naibu
Kamishna wa Magereza, Fidelis Mboya alipoulizwa kuhusu hali hiyo, licha
ya kukiri, alisema asingependa kueleza kwa undani mpaka apelekewe
maswali kwa maandishi.
“Nitumie maswali kwa maandishi ili na mimi
nijibu kwa maandishi, hili jambo ni ‘very sensitive’ (nyeti sana), lete
maswali nitakujibu kwa maslahi ya taifa,” alisema Mboya.
Matukio ya utata wa umri Suala
la umri wa watuhumiwa na hata wafungwa limekuwa gumzo katika siku za
hivi karibuni baada ya mawakili wa mwigizaji wa filamu, Elizabeth
Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii
mwenzake Steven Kanumba, kuwasilisha ombi lao Mahakama Kuu ikitaka
iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto kwa
madai kuwa mteja wao bado ni mtoto.
Uamuzi huo ulikuja baada ya awali, kugonga mwamba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Lakini,
tayari katika Bkutano wa Bunge la Aprili 14, 2010 aliyekuwa Mbunge wa
Viti Maalumu (CUF), Mgeni Jadi Kadika wakati akiuliza swali alitaka
kujua Serikali haioni kuwa kuna ulazima watoto kujengewa magereza yao au
kuwekwa sehemu maalumu.
Alisema hilo linatakiwa kufanyika kwa
kuwa watoto hao wanapokuwa gerezani hukutana na wafungwa wenye tabia
mbalimbali kama wizi, ubakaji, ujambazi na kwamba watoto hao wanaweza
kuiga tabia hizo.
Akijibu swali hilo aliyekuwa Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki alisema kwa mujibu wa Sheria
zinazoratibu, kuongoza na kusimamia masuala ya mahabusu, wafungwa watoto
wanapopelekwa magerezani wanapaswa kutenganishwa na wakubwa.
Kagasheki
alinukuu Kanuni za Uendeshaji wa Jeshi la Magereza (The Prisons
Standing Orders) ya 2003, Kifungu Namba 502, vifungu vidogo vya (ii) na
(iii), wafungwa watoto wanapopelekwa magerezani wanatenganishwa na
wafungwa wakubwa.
|
|
No comments:
Post a Comment