MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imechukua jukumu la kufanya uchunguzi wa
umri wa muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu,
anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya aliyekuwa muigizaji mwenzake Steven
Kanumba.
Mahakama hiyo ilitoa uamuzi huo jana kufuatia maombi
yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea
mshtakiwa huyo likiongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama.
Lulu
ambaye anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
umri wake ulizua mvutano baina ya mawakili wanaomtetea kwa upande mmoja
na upande wa mashtaka(Jamhuri na pamoja na Mahakama ya Kisutu kwa upande
mwingine.
Mawakili wa mshtakiwa huyo walidai kuwa mshtakiwa huyo
bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya
mashtaka inavyosomeka na kwamba na maana hiyo anapaswa kushtakiwa katika
Mahakama ya Watoto (Juvenile Court).
Katika maombi hayo namba 46
ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa Mahakama Kuu Mei 15 na mmoja wa mawakili
wake, Peter Kibatala walikuwa wakiiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama
Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali
wa msanii huyo.
Waliiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.
Akitoa
uamuzi wa maombi hayo jana Jaji Dk Fauzi Twaib alitengua na kutupilia
mbali uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi kukataa kuwa haina uwezo wa
kushughulikia maombi hayo, akisema kuwa mahakama hiyo ilikosea.
Akirejea
uamuzi ya Mahakama Kuu katika kesi mbalimbali zenye mazingira sawa na
kesi hiyo, Jaji Dk, Twaib alielezea kushangazwa kwake na Mahakama ya
Kisutu kukataa maombi hayo akisema kuwa ilikosea kwa kuwa ina mamlaka ya
kuyashughulikia.
Jaji Dk Twaib pia alikubaliana na hoja za
upande wa Jamhuri walizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kuwa
maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo isivyo halali kwa mujibu wa
sheria. Alisema kifungu cha 100 (2) cha Sheria ya mtoto ya mwaka
2009 kilichotumiwa na upande wa waombaji hakikustahili kwa kuwa hakuna
shauri liloko mbele ya mahakama hiyo kama kifungu hicho kinachoelekeza
bali shauri hilo liko Mahakama ya kisutu.
Kutokana na mazingira
hayo Jaji Dk Twaib alisema kuwa kuna njia mbili ambazo moja ni
kuwasilisha upya maombi hayo mahakamani hapo na ya pili ni mahakama hiyo
kutumia mamlaka yake chini ya Kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za
Hakimu Mkazi kujiridhisha usahihi wa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu. Alisema
kulingana na unyeti wa kesi hiyo Mahakama Kuu kwa kutumia mamlaka yake
na kwa kuzingatia kifungu cha 44 cha Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi
imeamua kufanya uchunguzi huo yenyewe.
Alisisitiza kuwa kulingana
na asili na unyeti wa mashtaka yanayomkabili mwombaji, kutokuwa na
uwezekano wa kupata dhamana na uharaka suala lenyewe kuhitaji uchunguzi
wa utata wa umri wake linahitaji uchunguzi wa haraka.
Aliongeza
kuwa kwa sababu hizo ameamua kutumia kifungu cha 44(1) cha Sheria ya
Mahakama za Hakimu Mkazi, ili Mahakama hiyo iweze kufanya uchunguzi wa
umri wa mshtakiwa huyo kama ilivyoombwa na waombaji.
Kutokana na
uamuzi huo pia Jaji Twaib kwa mamlaka ya mahakama hiyo aliamuru mwenendo
wa kesi hiyo katika Mahakam ya Kisutu usimame kusubiri kumalizika kwa
uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo.
Sambamba na uamuzi huo Jaji
Twaib aliamuru upande wa waombaji kuwasilisha mahakamani hapo hati ya
kiapo na nyaraka za ushahidi wa umri wa mteja wao kesho.
Pia
aliauagiza upande wa wajibu maombi (Jamhuri) kuwasilisha mahakamani
ushahidi wowote kuunga mkono msimamo wake Juni 20, 2012 na Juni 22, 2012
muombaji awasilishe majibu ya ufafanuzi (Rejoinder) na akaamuru maombi
hayo kusikilizwa Juni 25, 2012.
|
|
No comments:
Post a Comment