Wednesday, July 18, 2012

Bonanza la wanahabari jijini arusha lawakutanisha ccm na chadema



MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Arusha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Catherine Magige na mwenzake Joyce Mukhya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), juzi walisahau tofauti zao za kiitikadi kwa wote kukubali ombi la kuwa walezi wa Chama Cha waandishi wa habari (TASWA), mkoa wa Arusha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye bonanza la waandishi wa habari mkoa wa Arusha zilizofanyika viwanja vya General Tyre juzi, wabunge hao waliwaasa vijana kushiriki michezo kwa sababu zaidi ya kujiweka sawa kimwili na kiakili, michezo pia ni ajira.
“Vijana wenye vipaji vya michezo mbalimbali vya michezo waache kukaa vijiweni kwa kisingizioa cha kukosa ajira, waendeleze vipaji vyao kwa kufanya mazoezi ili wapate ufanisi itakayosaidia wao kujiajiri kupitia michezo,” alisema Magige aliyekuwa mgeni rasmi kwenye bananza hiyo.
BAADHI WANAHABARI WAKIWA WANAFWATILIA MICHEZO KWA UKARIBU WAKATI WA BONANZA LA WANAHABARI JUMAPILI JULAI 15, 2012

Ili kuimarisha mfuko wa TASWA wa kuendeleza vipaji vya michezo mkoani Arusha, wabunge hao kila mmoja alichangia Sh milioni moja huku wakiahidi kutumia nafasi zao na fursa zitakazopatikana kuhimiza watu wengine wenye uwezo kuchangia mfuko huo.

Kwa upande wake, Mukhya aliwaasa mamia ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari na vyuo vya Uandishi wa habari mkoani Arusha, kutumia taaluma yao kusaidia kusukuma mbele harakati za maendeleo kwa kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo.

“Arusha kuna fursa nyingi lakini wananchi hawapati taarifa sahihi kuhusu fursa hizo. Hii changamoto kwa vyombo vya habari kuvitangaza fursa hizo ili wananchi wazitumie kujikwamua kiuchumi,” alisema Mukhya.

Timu ya wanafunzi wa Uandishi wa habari kutoka Chuo cha Arusha Journalism Training College (AJTC), kiliibua kidedea katika mchezo wa soka na netiboli ambapo upande wa soka walinyakua zawadi ya Sh 250,000 wakati netiboli walipata Sh 100,000.

Mfungaji bora katika bonanza hiyo, Jeremia Frank kutoka AJTC alijinyakulia dola 110 za Kimarekani zilizotolewa na aliyekuwa diwani wa Kata ya Kaloleni kupitia Chadema aliyevuliwa uanachama, Charles Mpanda aliyetoa dola 10 wakati mbunge Magige alitoa dola 100.

Michezo mingine ilivutia washiriki ni kufukuza kuku, kuvuta kamba na kukimbia kwa magunia.

Timu ya waandishi wa habari iliyojumuisha wanaume kwa wanawake ilifungwa kwa taabu goli 4-0 na timu ya Kiwanda cha bia nchini, TBL.
SOURCE:  http://pamelamollel.wordpress.com

No comments:

Post a Comment