Thursday, September 13, 2012

Maandamano dhidi ya filamu ya kuukashifu Uislamu yasambaa

Maandamano dhidi ya filamu ya kumkashifu Mtume Muhammad mjini Tunis, Tunisia.
Maandamano ya Waislamu yameenea sehemu nyingi duniani wakipinga filamu iliyotengenezwa Marekani na inayomkashifu Mtume Muhammad, ambapo polisi wa Cairo wametumia mabomu ya machozi kutawanya waandamanaji hao. 

Rais wa Muhammed Mursi wa Misri ametoa baraka za kufanyika kwa maandamano ya amani lakini akasema ni kinyume kuwaua raia na kushambulia balozi. "Kutoa maoni, uhuru wa kuandamana na kutoa misimamo ni jambo ambalo linakubaliwa lakini pasipo kuharibu mali na balozi." Amesema Rais Mursi kupitia televisheni ya nchi yake huku pia akilaani mauaji ya balozi wa Marekani nchini Libya na kuahidi kulinda wageni.

Wizara ya afya ya Misri imesema watu kumi na tatu wamejeruhiwa katika maandamano hayo ambapo waandamanaji wameshusha bendera ya Marekani na kuichoma na kisha kupandisha bendera nyeusi.
Serikali ya Misri imetoa wito kwa raia wake kurejesha amani huku pia ikiikosoa filamu hiyo ambayo imeleta hasira nchini Libya na kusababisha vifo vya raia wanne wa Marekani akiwemo Balozi Chris Stevens mjini Benghazi.


Katika taarifa ya baraza la mawaziri iliosomwa na Waziri Mkuu Hisham Qandil , uongozi wa nchi hiyo umesema filamu hiyo imemdhalilisha Mtume Muhammad na pia imekiuka maadili. "Tunawaomba wananchi wote wa Misri kueleza hasira zao kwa amani," imeeleza sehemu ya tamko hilo.

No comments:

Post a Comment