Rais wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi jana ameimarisha kampeni yake ya kutafuta uungaji mkono wa Ujerumani kuhusu mpango wa kukabiliana na mgogoro wa madeni katika benki hiyo, kwa kuwaambia wabunge mjini Berlin kuwa mpango wa benki hiyo wa kununua hati za dhamana utasaidia kuondoa hofu kuhusu mgoro wa sarafu ya euro.
Draghi ameuambia mkutano wa pamoja wa kamati tatu za Bunge la Ujerumani, kwamba mpango huo wa kununua hati za dhamana hautachochea ughali wa maisha wala kuhujumu uhuru wa benki kuu ya Ulaya.
Aliongeza kuwa ununuzi wa hati za dhamana siyo hatua ya benki kuu ya Ulaya kusaidia kufadhili serikali za nchi wanachama, wala kusababisha athari nyingi kwa walipa kodi katika kanda ya sarafu ya euro.
Mkutano huo wa Draghi, na wanachama wa kamati za fedha, bajeti na masuala ya Ulaya, ambao watahitajika kutathmini jibu la Ujerumani kwa mgogoro huo, ulifanywa faraghani.
Mkuu huyo wa benki kuu ya Ulaya pia anatarajiwa kuulizwa maswali na wabunge kuhusu mgogoro wa kiuchumi unaoikumba Ugiriki.
No comments:
Post a Comment