Naibu jaji mkuu wa Kenya, Nancy Baraza, amejiuzulu baada ya tume iliyoundwa kuchunguza madai kuwa alimtishia mlinzi na bunduki, kupendekeza afukuzwe kazi.
Jaji Baraza amesema leo kuwa rufaa yake dhidi ya mapendekezo ya tume hiyo, aliyoiwasilisha katika mahakama ya rufaa isingesikilizwa kwa haki.
Alisema Jaji mkuu, ambaye pia ndiye rais wa mahakama hiyo, aliunga mkono mapendekezo ya tume hiyo katika mahojiano na kituo cha Televisheni, na kwa hivyo asingeweza kumtendea haki katika rufaa yake.
Ameongeza kuwa majaji wengine wawili kutoka mahakama ya rufaa walipendekeza kuundwa kwa tume hiyo kumchunguza.
Tume hiyo ya wajumbe saba iliyoongozwa na jaji mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhani, iligundua kuwa mkesha wa kuamka mwaka mpya 2012 Baraza alitishia kumpiga risasi Rebecca Kerubo, mlinzi katika kizuizi cha usalama cha duka moja kubwa jijini Nairobi.
No comments:
Post a Comment