Watu wasiopungua 44 wameuawa katika shambulio la angani dhidi ya mji unaodhibitiwa na waasi wa Maaret-al Numan nchini Syria.
Wafanyakazi wa uokozi wamemwambia mwaandishi wa habari wa shirika la habari la AFP aliyekuwepo katika eneo la tukio kuwa wamegundua miili 44 kutoka kwenye vifusi.
Kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja wa misaada, shambulio hilo kutoka kwa majeshi ya Syria, liliyaharibu majengo mawili ya makaazi na msikiti ambako wanawake wengi na watoto walikuwa wamekimbilia kupata hifadhi.
Mjumbe wa kimataifa wa amani nchini Syria, Lakhdar Brahimi ameziomba pande mbili zisitishe mapigano wakati wa siku kuu ya Eid el-Hajji, nafasi ambayo amesema inaweza kuweka msingi wa kuleta amani ya kudumu.
Shirika la habari la Syria, SANA liliripoti kuwa waasi waliripua bomba za kusafirisha mafuta na gesi kaskazini mashariki mwa Syria, karibu na Iraq.
No comments:
Post a Comment