Mjumbe wa amani kuhusu Syria Lakhdar Brahimi amesema leo kuwa serikali ya Syria imekubali kutekeleza pendekzo lake la usitishwaji wa muda mapigano wakati wa sherehe za kiislamu ya siku nne kuanzia Ijumaa.
Hata hivyo Syria imesema kuwa jeshi lake bado linatathmini pendekezo hilo na uamuzi wa mwisho utatolewa kesho Alhamisi. Taarifa ya Syria iliziweka katika hali isiyoeleweka juhudi za Brahimi za kusitisha kwa muda, umwagikaji wa damu nchini humo, wakati waasi wanaopigana kumwondoa madarakani rais Bashar al Assad wakikosa kuonyesha dalili yoyote kuwa wako tayari kusitisha vita.
Akizungumza katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo, Brahimi alisema kuwa baada ya ziara yake mjini Damascus, kuna makubaliano kutoka kwa serikali ya Syria ya kuweka chini silaha wakati wa siku kuu ya Eid.
Lakini Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Syria imesema pendekezo hilo bado linajadiliwa na uongozi wa kijeshi. Wakati huo huo ndege za kivita za Syria zimefanya mashambulizi mengine ya angani katika mji ambao ni ngome ya waasi wa Maarat al Numan, huku waasi wakiizingira kambi moja ya kijeshi mashariki mwa mji huo. Watu watano kutoka familia moja, akiwemo mtoto na mwanamke mmoja waliuawa katika mashambulizi hayo ya angani.
No comments:
Post a Comment