Sheikh Ponda Issa Ponda, akifunguliwa pingu, baada ya kufikishwa kwenye chumba cha mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana Alhamisi Novemba 1, 2012.
Kiongozi huyo mwenye msimamo mkali, alifikishwa kwa mara ya pili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na wafuasi wake ambapo hakimu anayesikiliza kesi dhidi yake, Victoria Nongwa, ya kuvamia eneo la Markaz, Chang'ombe jijini Dar es Salaam, ambapo waliharibu na kuiba mali mbali mbali zenye thamani ya shilingi milioni 59, madai ambayo washtakiwa wote waliyakanusha.
Hakimu huyo alikubali kutoa dhamana kwa washtakiwa wote isipokuwa kiongozi huyo ambaye ni mshtakiwa namba 1 kwa madai kuwa bado Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hajaondoa pingamizi lake la kuzuia dhamana kwa mshtakiwa namba moja.
Ulinzi katika mahakama hiyo ulikuwa ni mkali na haujawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni, ambapo pamoja na mambo mengine, palifungwa CCTV Cameras, vifaa vya kugundua vitu vyenye asili ya chuma, polisi wa kutuliza ghasia magereza na wale wa FFU, polisi wa farasi na mbwa, pamoja na askari kanzu waliotapakaa kila kona ya maeneo ya jirani na mahakama hiyo kubwa jijini Dar es Salaam.
Kikundi kidogo cha wafuasi wa Sheikh Ponda, kilijaribu kuleta rabsha, lakini polisi walitumia busara na kuwaelekeza kilichoamuliwa mahakamani ambapo pamoja na kusuasua kuondoka eneo hilo la mahakama, lakini hatimaye waliondoka huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwafuata kwa nyuma hadi eneo la makutano ya barabara za Bibi Titi na ile ya Morogoro nao wakatawanyika.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari, kulikuwepo taarifa kuwa wafuasi hao walipanga kutega milipuko kwenye eneo la mahakama na pia walisambaza vipeperushi vyenye vitisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano makubwa ya kulazimisha kiongozi huyo aachiliwe. |
No comments:
Post a Comment