Thursday, February 7, 2013
ASKOFU THOMAS LAIZER WA KKKT DAYOSISI YA KASKAZINI KATI AFARIKI
Habari zilizotufikia hivio punde kutoka Jijini Arusha zinaarifu kuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Ask Thomas Laizer amefariki dunia.
Taarifa hizo zinadai kuwa Ask. Laizer amefikwa na umauti alasiri ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya Selelian ya Mjini Arusha.
Jana Februari 6, 2013 Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alimtembelea na kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Taarifa zilipasha kuwa Askofu Laizer alilazwa Hospitalini hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja, na hakuna daktari wala ndugu aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.
Pinda alikwenda hospitalini hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Hata hivyo, baada ya kutoka katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi kuzungumzia hali ya mgonjwa, Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na kulikuwa na ulinzi mkali ambapo pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye.
Awali ilisemekana kuwa Askofu Laizer amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya watu wengi kumiminika Selian kutaka kumwona, lakini jana ilidhihirika kuwa, amelazwa hospitalini hapo.
sambweti blog inatoa pole kwa Waumini na washarika wote wa KKKT nchini kote kufuatia msiba huo mzito ulilolikumba Kanisa la Kilutheri hasa wakati huu ambao kuna mgongano kati ya waumini na Viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment