Sunday, June 16, 2013

Mandela aendelea kupata nafuu hospitalini


Mzee Nelson Mandela

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela anaendelea kupata nafuu, katika hospitali moja nchini Afrika Kusini.
Mandela ambaye amelazwa katika hopistali kwa siku ya nane, amekuwa akipokea matibabu kufuatia maambukizi ya mara kwa mara ya mapafu.
Mjukuu wa rais huyo wa zamani Mandla Mandela amesema Mzee Madiba yuko buheri wa afya na hali yake inaendelea kuimarika.

Mandela alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini mwaka wa 1994, baada ya kuongoza harakati za kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi, kwa miongo kadhaa.
Mandela alistaafu rasmi baada ya kuiongoza Afrika Kusini kwa kipindi cha miaka mitano.
''Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa raia wote wa Afrika Kusini na kote ulimwenguni, madaktari na maafisa wa chama tawala cha ANC kwa maombi yao na msaada wanaotoa kwa familia ya Mzee Mandela'' Alisema Mandla.
Matamshi ya Mandla yanaonekana kuwiana na taarifa iliyotolewa na serikali ya Afrika Kusini siku mbili zilizopita, kuhusiana na afya ya Mandela.
Nelson Mandela amekuwa katika chumba cha wagojwa mahututi tangu alipolazwa hospitalini siku nane zilizopita.
Jamii ya Kimataufa imekuwa ikifuatilia afya ya rais huyo wa zamani ambaye anatimu umri wa miaka tisini na tano mwezi ujao kwa karibu.
Mkewe Mandela, Graca Machel amekuwa akimtembelea mumewe hospitalini mara kwa mara na wki iliyopita alihairisha ziara yake ya kwenda Uingereza ili kuwa karibu na mumewe anayeugua.
Desemba mwaka uliopita, Bwana Mandela alilazwa hospitalini kwa siku kumi na nane kufuatia maambukizi ya mapafu na uvimbe kwenye kibofu cha mkojo.

No comments:

Post a Comment