Sunday, June 16, 2013

Watanzania watakiwa kuiunga mkono Taifa Stars dhidi a Ivory Cost hii leo



Kikosi cha Timu ya Taifa, Kilimanjaro Stars, itakayopambana na Ivory Coast kuwania pointi muhimu kwa ajili ya kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Brazil mwakani

Na Mwandishi Wetu
WADHAMINI wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Kilimanjaro Premium Lager, wamewaomba Watanzania washikane na kuungana pamoja wakati wa mechi dhidi ya Ivory Coast kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwani wapo waliokata tamaa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, alisema Stars inatakiwa kuungwa mkono na kushangiliwa kwa nguvu kwani wachezaji wameonesha kuwa wana uwezo.

"Hawa ni wanajeshi wetu, nawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi, tuwape sapoti na tuoneshe uzalendo kwani kwenye soka lolote linawezekana," alisema Kavishe.

Alisema Watanzania lazima waelewe timu bado ni changa na ina wachezaji wapya wenye umri mdogo, ambao wameonesha uwezo mkubwa.

"Hata ikitokea tusifuzu kwenda Kombe la Dunia, vijana wameshaonesha dalili nzuri na tuna imani tutafanya vizuri katika mashindano mengine kama AFCON na CHAN," aliongeza.

Kavishe aliwataka wachezaji kutulia uwanjani na kutobabaishwa na ukubwa wa timu ya Ivory Coast kwani wana uwezo wa kuwafunga na kushangaza dunia leo jumapili

"Hii ni kama fainali kwa Ivory Coast na wao pia wamebabaika na kuitilia maanani mechi hii kwa sababu tukiwafunga ina maana hawatakuwa na uhakika wa kufuzu katika hatua inayofuata," alisema meneja huyo.

Bia ya Kilimanjaro Premium Lager imetimiza mwaka mmoja tangu ianze kuidhamini Taifa Stars, na wadau mbalimbali wamesifu udhamini huo kwani umeleta mabadiliko katika timu ya Taifa.

Ivory Coast iliwasili nchini Alhamisi usiku na imeweka kambi katika hoteli ya Bahari Beach, Kunduchi, tayari kwa mechi itakayopigwa katika Uwanja wa  taifa  leo jioni.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), maandalizi yote yamekamilika na mechi hii inatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya Watanzania watakaojitokeza uwanjani na kupitia runinga pia.

Ivory Coast inaongoza katika Kundi C ikiwa na pointi 10, Tanzania ya pili na pointi 6, Morocco ya tatu na pointi 5 na Gambia ni ya nne ikiwa na pointi 1.

No comments:

Post a Comment