Thursday, June 27, 2013

Ruzuku ya uendeshaji wa shule za msingi

Fedha za ruzuku 2013 – kiasi kikubwa cha fedha kinaripotiwa kufika shuleni
Lakini wazazi wengi hawajui ni kiasi gani shule inapaswa kupokea


Kiasi cha fedha za ruzuku kilichopokelewa katika robo ya kwanza tu ya mwaka 2013 kinaripotiwa kuwa karibu sawa na wastani uliogawiwa kwa mwaka mzima katika miaka mitatu iliyopita. Kati ya 2010 na 2012, shule zilipokea wastani wa TZS 2,202 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka badala ya TZS 10,000 zilizotajwa katika sera. Lakini katika robo ya kwanza ya mwaka 2013, shule zimeripotiwa kupokea TZS 2,094. Ingawa kiasi hiki bado ni chini ya kiasi cha robo moja katika TZS 10,000, bado hili ni ongezeko kubwa kulinganisha na miaka iliyopita. Kama mwenendo huu ukiendelea tunaweza kushuhudia upelekwaji wa kiasi kamili cha fedha za ruzuku katika mwaka 2013.

Hata hivyo, wazazi wanashindwa kufuatilia kuhusu fedha hizi kwani 8 kati ya 10 hawajui ni kiasi gani cha fedha za ruzuku kinapaswa kutolewa kwa kila mwaka. Miongoni mwa walimu wakuu, kwa upande mwingine, ufahamu wao uko juu zaidi, ambapo zaidi ya nusu (asilimia 54) waliweza kutaja kiasi kamili ambacho kila shule inastahili kupokea kwa kila mwanafunzi.

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti unaoitwa Fedha za ruzuku katika shule za msingi: Muongo mmoja tangu kuanzishwa, je, fedha zinafika shuleni? Muhtasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, ambao ni mradi wa kitaifa wa utafiti kwa njia ya simu za mkononi unaohusisha kaya tofauti, kote Tanzania Bara.

Matokeo ya hivi karibuni ya vijana wa sekondari waliohitimu Kidato cha Nne yameibua mjadala wa kitaifa kuhusu ubora wa elimu nchini Tanzania. Fedha za ruzuku, ambazo zilianza kutolewa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) mwaka 2002. Mpango huu ulibuniwa ili kukuza ubora wa huduma hiyo ya msingi. Kwa namna mahususi kabisa, fedha zilikusudiwa kuziwezesha shule za umma kununua vitabu na zana nyingine za kufundishia na kujifunzia, kugharimia matengenezo madogomadogo,utawala na gharama za mitihani. MMEM pia unatoa sheria na kanuni zinazopaswa kufuatwa na shule ili kuhakikisha uwepo wa uwazi na ufanisi katika matumizi haya ya fedha

Shule zinapaswa kuwa na mwongozo unaotoa sheria za matumizi ya fedha za ruzuku, asilimia 95 ya walimu wakuu waliripoti kwamba shule zao zilikuwa na mwongozo huo;
Idadi kubwa ya walimu wakuu (asilimia 88) waliweza kutaja kiasi cha fedha za ruzuku kilichopaswa kutumiwa kununua vitabu kwa mujibu wa maelekezo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Shule zinapaswa kuwa na mbao za matangazo kwa umma ili kubandika taarifa za jinsi walivyotumia fedha za ruzuku, asilimia 80 ya shule zinafanya hivyo.

Matokeo haya yanaonyesha kwamba shule zina uelewa na uwezo wa kusimamia matumizi ya fedha za ruzuku kama inavyostahili. Hata hivyo, karibu theluthi mbili ya walimu wakuu (asilimia 63) walitoa taarifa kuwa hawakuridhishwa na mwenendo wa utoaji wa fedha za ruzuku. Zaidi ya hilo, karibu walimu wakuu wote (asilimia 93) waliripoti kwamba shule zao zilikuwa zinakabiliwa na uhaba wa vitabu.

Lakini walimu wakuu hawajabweteka. Karibu wote wameeleza kufuatilia suala la fedha za ruzuku pale zinapokuwa hazijapokelewa, kwa Maofisa Elimu wa Wilaya, Kamati za Shule na Kamati za Vijiji, miongoni mwa nyinginezo. Ni asilimia 17 tu ya wahojiwa ndio waliosema kwamba hawafuatilii.

Elvis Mushi, Mtafiti wa Twaweza, alieleza kuhusu matokeo hayo: “Licha ya matokeo haya yanayoelekea kuwa chanya mwaka huu, ni wazi kwamba kiasi kilichokusudiwa hakifiki shuleni kwa ukamilifu na kwa wakati. Walimu wakuu wanajitahidi kufuatilia na kuzisaidia shule zao kuendelea lakini shule bado hazipati mahitaji kikamilifu na bado zina kazi ngumu katika kukuza ubora [wa elimu?]."

Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema “Suala kubwa ni uwazi. Wazazi, walimu, na umma kwa ujumla wanapaswa kujua nini kinaendelea. Hatuna budi kufuatilia: je, kuna kiasi cha kutosha katika bajeti? Je, zinakwama katika ngazi ya halmashauri za wilaya? Je, zinatumiwa sawasawa katika ngazi ya shule? Kama taarifa zote hizi zingewekwa mtandaoni na kwenye simu za mkononi, kila raia, kuanzia yule wa kawaida hadi Rais angeweza kusaidia watoto wetu kupata kile wanachostahili.”

Muhtasari huu wa Twaweza unatoa vilevile matokeo mengine na unaweza kupakuliwa kutoka mtandaoni kupitia www.twaweza.org/sauti

No comments:

Post a Comment