Moses Mashalla, Arusha MADIWANI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Arusha
wamechafua hali ya hewa kwa kususia uchaguzi wa Naibu Meya Halmashauri
ya Manispaa ya Arusha, kitendo kilichosababisha uchaguzi huo kukwama kwa
mara nyingine.
Hatahivyo, katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya
maofisa wa Usalama wa Taifa pamoja na askari wa Jeshi la Polisi wakiwa
na magari yao, jana walionekana kwa wingi wakirandaranda nje na ndani ya
ofisi hizo kitendo kilichoibua maswali mengi.
Akifungua kikao
cha Baraza la Madiwani kabla ya kuanza kujadili ajenda mbalimbali za
kikao hicho, Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo alisema anashangaa ni kwa
nini madiwani wa Chadema wasusie kikao hicho wakati walikubali mwafaka
na kumtambua yeye kama meya.
Pia, alisema awali madiwani hao walikubali mwafaka ili wawaletee maendeleo
wananchi lakini alihoji watu hao hao waliokubali mwafaka leo hii
kususia vikao na kumtishia maisha huku wengine wakisema hawamtambui yeye
kama meya.
Lyimo, alisema kuwa kikao hicho kilikuwa na ajenda
tatu muhimu ambazo ni kuchagua wenyeviti wa kamati mbalimbali, kupitia
taarifa za mapato na matumizi pamoja na uchaguzi wa Naibu Meya, ambaye
alitakiwa kutoka Chadema, lakini cha ajabu chama hicho hawajaleta jina
wala kuhudhuria kikao hicho.
Alisema kutokana na madiwani wa
Chadema ambao ni saba kususia kikao hicho walikubaliana na madiwani wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuachana na ajenda hiyo mpaka kikao cha
dharura kitakapoitwa kujadili suala hilo.
“Kikao hiki kina
washiriki 23 ambapo watano kati yao ni wabunge na 18 ni madiwani, ila
kwa leo wapo madiwani 12, tumefika nusu ya kolamu, ila madiwani wa
Chadema wameandika barua na kueleza sababu zao za msingi za kususia
kikao hiki kuwa wanataka uchaguzi wa Meya ufanyike tena na kuitaka
Serikali kukubali uchaguzi urudiwe ili apatikane Meya halali ndipo wao
washiriki,” alisema Lyimo.
Alisema barua hiyo waliyoandika Chadema na kuipeleka kwa Mkurugenzi
wa Manispaa ya Arusha, pia ilikuwa na ikitishia maisha watu iwapo
hawatafanya uchaguzi wa Meya, jambo ambalo siyo halali.
Alisema kuwa, anakishangaa chama hicho, iwapo kama wameona hawakutendewa
haki, mahakama ndiyo sehemu ya kukimbilia, ambako hawataki kwenda
badala yake wanagoma na kuwatishia watu maisha na kusisitiza ni Mungu
pekee ndiye anayekuwa mlinzi wa watu aliyewaumba.
Lyimo alisema,
anakumbuka walifanya kikao Juni 20 mwaka jana 2011 na pande hizo mbili
na kukubaliana mwafaka na kuwapa nafasi ya Naibu Meya Chadema, ila
anashangaa kuona wamegeuka makubaliano hayo.
Alisema kikubwa kilichopo ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo kulumbana, kwa sababu hawakuchaguliwa kuendesha malumbano.
Upande
wa madiwani wa CCM, wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Olasiti, Ismail
Katamboi alisema kuwa, kwa sababu Chadema wamekataa kuleta jina la Naibu
Meya wamevunja kanuni na maazimio ya mwafaka wao ambao walikaa na
kupongezana basi iwekwe katika kikao kijacho kama ajenda na watoe uamuzi
wao.
Hali hiyo ilimlazimu, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Omary Mkombole
kusimama na kuingilia kati na kuwataka madiwani kuacha kujadili suala
hilo kwani siyo kikao cha kujadili suala la mwafaka na kushauri madiwani
hao kujadili suala hilo kikao kijacho kitakachoitwa kwa dharura.
Naye
mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema, Isaya Doita, alitoa tamko kwa niaba
ya madiwani wenzake saba kuwa hawatashiriki uchaguzi wa Naibu Meya kwa
kuwa uongozi wa chama hicho ngazi ya Wilaya ya Arusha uliandika
barua Julai 14 mwaka huu, yenye kumbukumbu nambari MD/E40/10/VOL 11 kwa
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo wakimtaarifu kutoshiriki uchaguzi huo na
kumtaka aitishe kikao cha uchaguzi wa Meya wa Arusha.
Alisema
Chadema hawawezi kuteua mtu kwa nafasi ya Naibu Meya wakati hawatambui
na kutaka uchaguzi wa meya ufanyike kwa kuwa manispaa hiyo haina meya
kwa sababu aliyepo alichaguliwa kinyume cha sheria.
Doita
alisema, baada ya kupeleka barua hiyo Ofisi ya Mkurugenzi Arusha
ilipokewa na Julai 16 mwaka huu, ilijibiwa na Kaimu Mkurugenzi, Mkombole
ambaye alisema kuwa kuhusu marudio ya uchaguzi hayuko tayari kwa
sababu ofisi yake inatambua kuwapo kwa meya aliyechaguliwa kihalali kwa
kufuata taratibu zote za kuendesha vikao.
Alieleza kwamba, barua
hiyo ilisema uchaguzi wa meya ulifanyika Desemba 17 na 18 mwaka 2010
ulifuata sheria na kanuni zote za manispaa na hivyo meya aliyepo kwa
sasa ni halali.
Chanzo na gazeti la Mwananchi
|
No comments:
Post a Comment