Saturday, July 21, 2012

Rais atangaza siku tatu za maombolezo


Rais Jakaya Mrisho Kikwete
 
Serikali imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jana na bendera zitapepea nusu mlingoti nchini kote.

Pia, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Alli Mohamed Shein na ameahidi kwamba serikali itafanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha ajali hiyo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.

“Kutokana na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais Jakaya Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo (jana).

Rais amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji inaendelea,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

   
Taarifa hiyo imeeleza kuwa meli ya MV Skagit iliyopinduka na kuzama katika eneo la Chumbe, Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290.

Ilieleza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.

Ilisema kazi hiyo ilifanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni binafsi. 

Aidha, mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa. 

Rais pia amempongeza Rais wa Zanzibar, viongozi wote wa ngazi mbalimbali, maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa namna walivyojipanga kushughulikia ajali hiyo.

Aidha, Rais Kikwete pia amewapongeza wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment