Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi kuingia kidato cha tano katika shule za Sekondari za Serikali na Vyuo vya Ufundi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi kuingia kidato cha tano katika shule za Sekondari za Serikali na Vyuo vya Ufundi. Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Edmund Kinuasi. (Picha ZOTE na Lorietha Laurence-
Na Belinda Kweka-MAELEZO
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema kuwa ufaulu wa wanafunzi kidato cha nne kuingia kidato cha tano umeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka jana.
Akiongea hayo Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo amesema kuwa jumla ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na na Kidato cha Tano pamoja na Vyuo vya Ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji mwaka huu ni wanafunzi 34,213,hii ni sawa na ongezeko la wanafunzi 2,790, ikilinganishwa na mwaka jana wanafunzi 31,423 walichaguliwa.
Amesema kuwa ongezeko hilo ni sawa na asilimia 8.9 ambapo jumla ya wanafunzi 33,683 wakiwemo wavulana 23,383 na wasichana 10,300 wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Tano katika shule za Serikali mwaka huu.
Mulugo ameongeza kuwa kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za Serikali, wavulana 13,708 na wasichana 5,262 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi.
“kwa ulinganisho wa kijinsi takwimu zinaonyesha kuwa wasichana ni wachache ikilinganishwa na wavulana waliofaulu kwa mwaka huu”, alisema Philipo Mulugo.
Aidha amesema jumla ya wanafunzi 76 waliokuwa na sifa za msingi za kujiunga na kidato cha tano hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo wanafunzi 5 kuwa na umri mkubwa na wanafunzi 70 wamekosa ‘combination’ na mmoja hakuwa raia wa Tanzania.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa Julai 29 mwaka huu wakati awali walikuwa wakiripoti aprili, wizara imezingatia taratibu zote za shule walizochagua kuwa zina ubora na mahitaji yote ya msingi kama vile maji, umeme, madarasa, bweni na vinginevyo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment