MAJAMBAZI jana yalifanya onesho la aina
yake jijini Dar es Salaam, baada ya kupora mamilioni ya shilingi
katika kituo cha mafuta cha Lake Oil, Buguruni Malapa na kumwaga fedha
hizo kwa wananchi maeneo ya Tazara ili kuhadaa polisi.
Wakiwa katika pikipiki aina ya Toyo na fuko la fedha, majambazi hao baada ya kupora fedha hizo, walifanikiwa kupita katika foleni ya magari mpaka katika taa za Tazara. Walipofika katika eneo hilo, ghafla polisi wenye silaha wakiwa katika pikipiki zaidi 10, walivamia na kusababisha majambazi hao kurusha sehemu ya fedha walizo pora hewani. Shuhuda mmoja wa tukio hilo, anayeuza bidhaa mbalimbali akiwa amebeba mkononi katika eneo la Tazara, alieleza gazeti hili kuwa walijikuta wakikimbilia fedha hizo, kitendo kilichosababisha polisi kushindwa kutambua majambazi hao
Kwa
mujibu wa shuhuda huyo, wakati wananchi wakigombea fedha hizo, huku
polisi wakihangaika kutaka kukamata watuhumiwa, majambazi hao walirukia
gari aina ya Suzuki Pick Up. Shuhuda
huyo alidai majambazi hao walimwamuru dereva kuondoka, lakini dereva
huyo alikumbwa na bumbuwazi, asijue la kufanya. Kutokana na kushindwa
kuondoka, papo hapo walimjeruhi kwa risasi. Muuza CD Mtu
mwingine ambaye alikuwa abiria katika gari hiyo, alipoona wamevamiwa,
aliruka na kuanza kutimua mbio kwenda upande wa soko la Vetenari. Hali hiyo ilisababisha polisi waliokuwa katika eneo hilo wakiwa na pikipiki, kuanza kumfukuza.
Gazeti
hili lilishuhudia zaidi ya pikipiki nne za polisi, waliokuwa wakipiga
risasi za moto hewani, wakimkimbiza abiria huyo, ambaye baadae alikutwa
katika soko la Vetenari, karibu na ukuta wa TBC na aligundulika ni
muuzaji wa CD za reja reja. Baada
ya muda mfupi, kundi la Polisi ambalo liliwasili katika eneo la tukio,
lilifanikiwa kuwadhibiti majambazi hao, ambao awali walidaiwa kuwa
watatu huku mmoja wao akiwa na silaha. Polisi
hao pia walionekana kuchukua fuko hilo la fedha na kuliingiza katika
moja ya magari sita, yaliyokuwa na polisi hao. Aidha, watuhumiwa hao
walipandishwa katika gari tofauti na lililobeba fedha hizo, huku
wakivuja damu.
Gari hilo
lilizungukwa na askari wa doria maalumu ya kudhibiti ujambazi jijini
Dar es Salaam. Mbali na magari hayo, pia pikipiki za Polisi zilikuwa
nyingi, jambo ambalo liliwatia moyo wananchi waliofika katika eneo
hilo, kuwashuhudia majambazi hao na wengine walisikika wakisema ‘Polisi
leo (jana) wamefanya kazi yao ipasavyo’.
Hata hivyo, wananchi hao walitaka wahalifu hao wasulubiwe papo hapo. Akizungumza
na gazeti hili, askari aliyekuwepo katika eneo hilo huku akikataa
kutaja jina lake, alisema wamekamata majambazi wawili, ambao walipora
fedha katika eneo la Buguruni Malapa na mmoja amekimbia. Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema
ofisi yake inakamilisha upelelezi, na leo taarifa kamili itatolewa
kupitia Kanda Maalumu ya Kipolisi
No comments:
Post a Comment