Friday, September 13, 2013

Kweli mapenzi mapenzi tu ona Mume amsamehe mkewe aliyepanga kumuua



Faith Wairimu Maina alitaka kumuua mumewe kufuatia madai kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine
Mwanamke mmoja mfanyabiashara mjini Nairobi, Kenya, ambaye alikiri kosa la kupanga njama ya kumuua mumewe, ameachiliwa na mahakama
Bi Faith Wairimu Maina, aliachiliwa huru baada ya mumewe kuitaka mahakama kufuta kesi yake kwani amemsamehe.
Bi Faith alikiri kuwa aliwakodi mamluki kumuangamiza mumewe. “Nataka kumsamehe kwa sababu ya watoto na familia yetu,” mumewe Faith aliambia mahakama.
Mwanamke huyo alikiri makosa ya kupanga njama ya kutaka kumuua mumewe baada ya kukamatwa ingawa baadaye alibadili msimamo wake na kukanusha madai hayo na alitarajiwa kushtakiwa.
Polisi walitibua njama ya mwanamke huyo baada ya majasusi waliokuwa wanajidai kuwa mamluki kupokea malipo ya shilingi 40,000 kuitekeleza njama hiyo.
Mwendesha mkuu wa mashtaka alisema kuwa alifahamishwa wanandoa hao walikubali kusameheana na kuwa bwana Muthee ambaye ni mumewe mwanamke huyo akataka kesi hiyo kufungwa.
Wakili wa mwanamke huyo alisema kuwa hakuwa na pingamizi zozote kutupilia mbali kesi hiyo. Bwana Muthee alisema kuwa mwanamke huyo ni mkewe na alimsamehe kwa sababu ya familia, jambo linaloruhusiwa na mahakama.
Mwanamke huyo tayari alikuwa amewalipa mamluki kumuua mumewe na kisha kuwataka wamletee nguo zake zenye damu ili aweze kuwalipa pesa zitakazokuwa zimesalia ambazo ni shilingi 160,000 na pia aweze kuthibitisha kuwa mumewe ameuawa.
Majajusi walisema kuwa ilikuwa mara ya pili kwa mwanamke huyo kujaribu kumuua mumewe baada ya njama ya kwanza kukosa kufaulu licha ya kuwalipa mamluki waliomwambia kuwa walishikwa na uoga.
Mwanamke huyo alipanga njama ya kumuua mumewe kutokana na madai kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine.

No comments:

Post a Comment