Sunday, November 24, 2013

CHRISTINA NEWA MMOJA WA MAJERUHI NA MLENGWA WA MAUAJI YA ILALA BUNGONI ASIMULIA TUKIO ZIMA LILIVYOTOKEA

MLENGWA wa shambulizi la mauaji lililotokea Novemba 19, mwaka huu  Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam, Bi. Christina Newa, ameibuka na kuwalaumu polisi kwa kushindwa kuzuia mauaji yaliyosababishwa na mpenzi wake, Gabriel Munisi. 

Katika tukio hilo Gabriel Munisi aliwashambulia ndugu wa familia moja na kuwaua watu wawili, Alpha Newa 'Nando' na shemeji yake Capt. Francis Shumila kabla ya yeye mwenyewe kujiua. 

Christina alifafanua kuwa licha ya kutoa taarifa za kutishiwa maisha katika kituo cha Polisi Kirumba jijini Mwanza na Pangani jijini Dar es Salaam, polisi walipuuza tishio hilo huku wakiwadhalilisha kwa kauli za kebehi.
Alisema uhusiano wake na Munisi haukuwa wa muda mrefu na kwamba baada ya kubaini kuwa kijana huyo ana tabia ya ukatili alifanya kila njia kuachana naye ikiwa ni pamoja na kwenda nchini Cyprus kwa ajili ya masomo.
Aliongeza kuwa akiwa nchini Cyprus Munisi alimpigia simu na kumuomba atakaporejea kwa likizo asiijulishe familia yake ili apate nafasi ya kumpokea
akiwa peke yake.
“Ni kweli niliporudi likizo Munisi alinipokea na alionekana kuwa mtu aliyebadilika kitabia na hata tukapanga safari ya kwenda Mwanza tuliongozana katika gari dogo lakini tukiwa sehemu moja ya Singida alinishusha na kunitolea bastola huku akiniambia nimueleze sababu ya kwenda kusoma nje bila kumtaarifu,” alisema Christina.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo alimuomba msamaha na  hali ikawa ya utulivu mpaka walipofika Mwanza huku Munisi akiwa amezuia kila kitu alichotoka nacho Cyprus ikiwemo Laptop.
Christina alisema kuwa hata hivyo hakuwa na wasiwasi na Munisi baada ya kuona amebadilika na kwamba katika hali hiyo alimuomba ruhusa ya kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya mambo  kabla ya kurejea jijini Mwanza.
Alisema akiwa jijini Dar es Salaam, Munisi alipeleka Laptop kwa mafundi kwa ajili ya kuondoa namba za siri na akaweza kuona picha zinazomuonyesha Christina akiwa ufukweni na wanafunzi wenzake jambo aliloeleza kuwa lilimkera na kuwa mwanzo wa mgogoro.
Huku akiushika mguu wake uliojeruhiwa kwa risasi Chrstina alisema, baada ya hali hiyo Munisi alianza kumpiga kila wakati huku akimfungia mlango asitoke nje mpaka atakaporudi  na kwamba hali hiyo ilidumu kwa muda mrefu mpaka alipopata msaada wa majirani walioweza kuwataarifu polisi na kumuokoa
Baba wa Munisi awatimua
 Chrstina alisema baada ya kipigo cha mara kwa mara alilazimika kufikisha malalamiko yake kwa mzazi wa  Munisi ambaye hakutaka kuwasikiliza na kumtaka aondoke nyumbani kwake.
Alisema kutokana na hali hiyo hakuwa na jinsi zaidi ya kurudi kwa Munisi na kuendelea kupokea manyanayaso mpaka siku alipopata msaada kutoka kwa mpita njia aliyewasiliana kupitia dirisha la nyumba yao.

 Christina alisema alimpa namba za mama yake mpita njia huyo ambaye aliwasiliana na mama wa Christina ambao walifika jijini Mwanza na kufanya mawasilino na Polisi wa Mwanza na kufanikiwa kumuokoa.

 “Siku Polisi walipokuja nyumbani, Munisi hakuamini kama wanamfuata kwa heri akanilazimisha tutoke pamoja nilikuwa na kanga tu mwilini na hapo ndipo tulipoanza safari ya kituoni kwa ajili ya kuandikisha taarifa,” alisema Christina.

Aliongeza kuwa wakiwa njiani kuelekea kituoni Munisi alipigia simu kwa ndugu wa Christina na kumtaka awaambie Polisi kwamba hakuna tatizo, jambo alilosema alilitekeleza kutokana na hofu aliyokuwa nayo.
Chrstina aliongeza kuwa baada ya kufikishwa kituoni alikataa kurudi kwa Munisi na ndipo akarejea jijini Dar es Salaam baada ya kutumiwa tiketi na ndugu zake.
Munisi amuwinda Dar
Alisema baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, Munisi alianza harakati za kutaka kupata msaada wa Polisi kutokana na vitisho vya Munisi ambapo alifika katika kituo cha Polisi Pangani na kutoa taarifa pasipo kupewa msaada wowote.

“Pale Pangani tulimkuta mpelelezi mmoja, huyu bwana alitusaidia mwanzo mpaka ndugu yetu aliporudi lakini kuhusu vitisho vya bastola, alisema hayo ni mambo ya mapenzi na hayawahusu,”.  Chrstina anasema baada ya kauli hiyo ya Polisi hawakuwa na njia ya kufanya na kuamua kutulia nyumbani kabla ya kubaini uwepo wa Munisi katika jiji la Dar es Salaam, aliyekuwa akifuatilia nyendo ya familia yao kila siku.
Alisema mara kwa mara Munisi alikuwa akimtumia ujumbe wa simu
na wakati mwingine kwenda kugonga katika nyumba yao na kumueleza kuwa hawezi kumuacha na kwamba ikitokea amemuacha atafanya mauaji katika nyumba zote tatu za familia hiyo
Siku moja kabla ya Mauaji.
Christina alisema siku moja kabla ya mauaji kutokea alipokea
ujumbe wa simu kutoka kwa Munisi ukimsifia kuwa amependeza hali iliyozidi
kumtia hofu na kuamua kumueleza shemeji yake Kapten Francis Shumila ambaye aliahidi
kumlinda.
“Nilimwambia Shemeji juu ya ujumbe wa Munisi naye akaniambia atanilinda na kama kufa ataanza yeye kabla ya kifo changu kumbe ndivyo alivyomaanisha,”alisema Chrstina kwa hisia kali.

Wakati wa Mauaji
Akisimulia hali ilivyokuwa muda mfupi kabla ya mauaji Christina alisema wakiwa wanatoka getini walimuona Munisi akiwafuata kwa kasi na kisha kutoa bastola hali iliyomfanya shemeji yake Kapten Shumila ashuke katika gari kwa ajili ya kutaka kumtuliza.

Alisema wakati Shumila akishuka katika gari Munisi alimfyatulia risasi ya kichwa na kisha risasi zingine akizielekeza katika gari na kumuua Dada wa Chrstina aitwae Alpha pamoja na kumjeruhi mama yao mzazi sehemu ya begani.
“Alikuwa kama Mnyama na katika hali hiyo niliweza kumsukumiza mama chini kwa ajili ya kumuokoa huku tukiwa tayari tumejeruhiwa na wengine wameshauawa Munisi kuona wote tumelala chini ndipo akajimaliza na bastola akidhani kwamba wote alishatumaliza,”alisema Chrstina.


CHANZO MICHUZI BLOG

No comments:

Post a Comment