Wednesday, November 20, 2013

MAHAKAMA YA RUFANI (T) KUONDOSHA JUMLA YA MASHAURI 188 KATI YA NOVEMBA NA DISEMBA, DSM, ARUSHA, MWANZA NA ZANZIBAR


Na Mary Gwera,Mahakama ya Tanzania

JUMLA ya Mashauri 188 yanatarajiwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi katika kipindi cha mwezi Novemba na Disemba kufuatia vikao (sessions) vya Mahakama ya Rufani (T) vilivyoanza rasmi wiki hii katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza pamoja na Zanzibar ambapo kikao chake kitaanza rasmi tarehe 02.12.2013.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Zahra Maruma katika taarifa yake juu ya kufanyika kwa vikao hivyo vya Mahakama hiyo na kubainisha kuwa miongoni mwa Mashauri yatakayosikilizwa yanahusisha mashauri ya Rufaa za jinai, madai pamoja na maombi mbalimbali ya Rufaa hizo.

Mhe. Maruma aliongeza kuwa kwa upande wa Arusha jumla ya Rufaa 45 zitasikilizwa na kutolewa maamuzi, 35 zikiwa ni Rufaa jinai (criminal appeal) na kumi (10) maombi ya madai (civil application).

Hata hivyo, Mhe. Maruma aliongeza kuwa katika Mkoa huo kesi hizo zitasikilizwa chini ya jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman wengine ni Mhe. Jaji Nathalia Kimaro, Mhe. Jaji Bernard Luanda na Mhe. Jaji Bethuel Mmila.

Alieleza katika taarifa yake kuwa kwa upande wa Dar es Salaam, ambapo kuna jumla ya mashauri 81 yaliyopangwa kufanyiwa kazi, yatasikilizwa na Majaji tofauti tofauti Kulingana na Kulingana na idadi ya kesi alizopangiwa kila mmoja, aliwataja Majaji hao kuwa ni Jaji Engela Kileo, Mhe. Jaji Sauda Mjasiri, Mhe. Jaji William Mandia wengine ni Mhe. Jaji Mbarouk Mbarouk na Mhe. Jaji Stephen Bwana.

Aliongeza kuwa, kwa upande wa Mwanza jumla ya mashauri 44 yatasikilizwa na kutolewa maamuzi pia, ambapo alitaja idadi ya mashauri ya Rufaa za jinai (criminal Appeal) kuwa ni 26 na maombi ya madai ( civil application) zikiwa 18.

Alisema kesi hizo zitasikilizwa chini ya jopo la Majaji watatu likiongozwa na Mhe. Jaji Edward Rutakangwa , Mhe. Jaji Semistocles Kaijage pamoja na Mhe. Jaji Kipenka Mussa.

Hata hivyo; Kaimu Msajili huyo aliongeza katika taarifa yake kuwa kikao kingine kinatarajia kufanyika Zanzibar tarehe 02.12. 2013 ambapo jumla ya mashauri 18 yakiwa ni Rufaa za jinai na madai yatasikilizwa na kutolewa maamuzi katika kikao hicho.

Alifafanua kuwa katika kikao hicho kitakachofanyika visiwani Zanzibar, kitakuwa na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Mhe. Jaji Mbarouk Mbarouk, Mhe. Jaji Bernard Luanda na Mhe. Jaji Ibrahim Juma.

Alieleza kuwa vikao (sessions) hivyo vyote vitakamilika rasmi mnamo tarehe. 13.12.2013, ambapo ametoa wito juu ya ushirikiano wa wa husika kwa lengo la kufanikisha kazi hii muhimu.

Mahakama ya Rufani (T) pamoja na Mahakama Kuu nchini imejiwekea utaratibu wa kusikiliza mashauri katika Mikoa mbalimbali lengo likiwemo ni kupunguza idadi ya mashauri katika Mahakama hizo Hali ambayo inalenga pia katika kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani.

No comments:

Post a Comment