Wednesday, January 8, 2014

NBS YATOA CHANGAMOTO KWA WATANZANIA KUANZISHA NA KUMILIKI VIWANDA ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA BIDHAA MBALIMBALI, AJIRA NA KUKUZA PATO LA TAIFA

Mkurugenzi wa Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke ametoa wito huo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es salaam kutoa taarifa ya fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani hadi kufikia mwaka 2012 zilizowekwa katika makundi mbalimbali kwa kufuata mwongozo wa Umoja wa Mataifa. 
Mtafiti na mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Haji Semboje akizungumza wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo mengine amesema juhudi zinahitajika katika kuwahamasisha Watanzania kumiliki viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa. 
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es Salaam.

Na Aron Msigwa, Dar es salaam.

WITO umetolewa kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi katika
kuanzisha na kumiliki viwanda vitakavyozalisha bidhaa
mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuongeza ajira, kukuza pato
la taifa na kupunguza hali iliyopo ya uagizaji wa bidhaa mbalimbali
toka nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke ametoa wito huo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo, jijini Dar es Salaam kutoa taarifa ya fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani hadi kufikia mwaka 2012 zilizowekwa katika makundi mbalimbali kwa kufuata mwongozo wa Umoja wa Mataifa.

Amesema kuwa ongezeko la viwanda nchini licha ya kuongeza
ajira kitakwimu lina mchango mkubwa katika kusaidia kupima
fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kuongeza  kuwa
uzalishaji wa bidhaa za viwandani hupima mabadiliko ya kiasi cha
bidhaa zilizozalishwa na wazalishaji mbalimbali ambao kwa
wastani wamejiajiri kuanzia wafanyakazi 50 na kuendelea.
Amefafanua kuwa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2006 hadi
2012 imekua na kiwango cha juu cha mabadiliko ya fahirisi ya bei
ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani kwa jumla ya asilimia 10.8
ikilinganishwa  na asilimia 2.1 za mwaka 2011.


Ameongeza kuwa fahirisi za uzalishaji wa bidhaa za viwandani
kwa mwaka 2012 zimeongezeka na kufikia 328 ikilinganishwa na
296 za mwaka 2011 na kuongeza kuwa ongezeko hilo
limechangiwa na uzalishaji wa vinywaji na tumbaku kwa asilimia
16.8%, Viwanda vya chuma 14.6% na ongezeko na bidhaa za nguo
na ngozi kwa asilimia -17.7%.


Bw. Oyuke ameyataja makundi mengine yatokanayo na bidhaa za
viwandani kuwa ni pamoja na Mbao na bidhaa za mbao 0.3%,
Karatasi na bidhaa za karatasi 5.0%, Kemikali, Petroli na bidhaa za
Plastiki -7.9%, Bidhaa za udongo, vioo na bidhaa zisizo za metaliki
7.5% na bidhaa zitokanazo na chuma 11.0% .


Naye mtafiti na mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
salaam Prof. Haji Semboje akizungumza wakati wa mkutano huo
amesema kuwa mfumo wa uzalishaji na biashara nchini unatokana
na uwepo wa bidhaa za Kilimo na zile zisizo kuwa za kilimo na
kuongeza kuwa juhudi kubwa zinahitajika katika kuwahamasisha
Watanzania kumiliki viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa.

“Bado tunakabiliwa na changamoto ya umiliki wa viwanda hapa
nchini kwa sababu viwanda vingi vikubwa vinamilikiwa na
wageni, watanzania walio wengi wanamiliki viwanda vidogo
vidogo” amesema Prof. Semboje.


Ameongeza kuwa hivi sasa kuna ongezeko kubwa la bidhaa
mbalimbali zikiwemo nguo kutoka nje ya nchi jambo ambalo
linaathiri uchumi wa ndani na kusisitiza kuwa kuwa juhudi
zinahitajika katika udhibiti wa bidhaa zisizokidhi viwango na
ambazo hazina chapa ya eneo zilikotengenezwa ambazo
zinapatikana katika masoko ya Tanzania.

Prof. Semboje ameeleza kuwa kutokana na kuongezeka kwa
uwezo wa watanzania kununua, kuagiza na kufanya biashara nje
ya nchi ipo haja ya watanzania hao  na serikali kwa ujumla kupitia
mamlaka husika za uwezeshaji wananchi kiuchumi kuangalia
uwezekano wa kuwajenga uwezo wa kununua mitambo
inayozalisha bidhaa hizo  na kuileta ndani ya nchini kwa lengo la
kuongeza pato la taifa na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Ninapenda kutoa wito kwa Taasisi za Uwekezaji nchini kutoa
kipaumbele kwa Watanzania katika suala la uwekezaji wa ndani
pia kutoa elimu zaidi kwa watanzania katika uzalishaji wa kisasa
kwa sababu tayari serikali imeshaweka mipango mizuri ya
kuwaendeleza watanzania, changamoto tuliyonayo ni kuitafsiri
mipango na sera zilizopo kwa manufaa ya nchi”.

No comments:

Post a Comment