Monday, February 24, 2014

VIONGOZI WA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI WAPEWA SEMINA ELEKEZI


Wakuu wa Majengo wakiwa na vyeti vyao mara baada ya mafunzo. Waliokaa kuanzia kushoto ni Bw. Godfred Mbanyi mwezeshaji kutoka Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi, akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Alois Njelekela, Dkt. Clemcence Tesha ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi akifuatiwa na Bi. Agnes Mtawa ambaye ni Mwenyekiti wa Tenda Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakuu wa Idara mbalimbali za Hospitali wakiwa na vyeti vyao mara baada ya mafunzo. Waliokaa kuanzia kushoto ni Bw. Godfred Mbanyi mwezeshaji kutoka Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi, akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Alois Njelekela, Dkt. Clemence Tesha ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi akifuatiwa na Bi. Agnes Mtawa ambaye ni Mwenyekiti wa Tenda Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakiwa na vyeti vyao mara baada ya mafunzo. Waliokaa kuanzia kushoto ni Bw. Godfred Mbanyi mwezeshaji kutoka Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi, akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Marina Alois Njelekela, Dkt. Clemence Tesha ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Watalaam wa Ununuzi na Ugavi akifuatiwa na Bi. Agnes Mtawa ambaye ni Mwenyekiti wa Tenda Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao ni Wakuu wa Idara, Mameneja wa Majengo, pamoja na baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Tiba ya Figo na Magonjwa ya Mtumbo wamepigwa msasa kuhusu menejimenti ya usimamizi wa Idara na Vitengo wanavyoviongoza. Wakuu hawa wa Idara na Mameneja wa Majengo wamechukua nafasi hizi mapema mwezi Januari 2014 zitakazodumu kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Mafunzo haya yalikuwa na mada kadhaa ikiwemo wajibu wa Wakuu wa Idara na Mameneja wa Majengo, Mawasiliano Rasmi ndani na  nje ya Taasisi,  Umuhimu na namna ya kufanya Tathmini kwa wafanyakazi walioko chini yao, mipaka yao katika kufanya kazi, namna ya kutengeneza mpango kazi wa mwaka uliotoolewa kwenye Mpango Mkakati wa Hospitali, jinsi ya kutoa adhabu kwa wafanyakazi pamoja na utaratibu unaotakiwa kufuatwa.

Aidha, Viongozi hawa walipata mafunzo kuhusiana na kanuni za fedha, utaratibu wa kuandaa bajeti na malipo,  umuhimu wao katika kubuni vyanzo vya mapato na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha, umuhimu wa kusimamia watendaji walioko chini yao ili kujaza kwa usahihi fomu mbalimbali za matibabu ya wagonjwa ikiwemo fomu za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na bima nyinginezo.

Mada nyingine ilihusu matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo Hospitali ya Taifa Muhimbili inatakiwa kuacha matumizi ya karatasi (paper less) ili kuwa mfano kwa Hospitali nyingine za umma hapa nchini.

Viongozi hawa walipata mafunzo pia kuhusiana umuhimu wa mawasiliano kati yao viongozi kwa viongozi, kati yao na wafanyakazi walioko chini yao na kikubwa zaidi umuhimu wa kuwasiliana na wateja wanaowahudumia ili kuhakikisha wanawapata taarifa sahihi kuhusu mienendo ya matibabu yao.

Aidha walipata fursa ya kujua utaratibu unaotumika katika kufanya manunuzi ya vifaa tiba, dawa pamoja na vitendanishi mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Hospitali katika idara wanazoziongoza.  

Kimsingi Viongozi hawa wanatoka katika Kurugenzi nane za Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo ni Kurugenzi ya Tiba yenye Idara saba ambazo ni (Idara ya Tiba, Magonjwa ya Dharura, Afya ya Watoto, Utengamano, Magonjwa ya Nje, Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili, na Idara ya Magonjwa ya Moyo ambayo ni idara mpya ikijumuisha kitengo cha upasuaji wa moyo).

Kurugenzi ya Upasuaji yenye Idara sita ambazo ni (Idara ya Upasuaji ikijumuisha Kitengo cha Upasuaji wa Watoto, Nusu Kaputi na Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Macho, Idara ya Afya ya Kinywa na Meno, Magonjwa ya Akina na Mama na Uzazi pamoja na Idara ya Pua Masikio na Koo.

Kurugenzi ya Tiba Shirikishi ina Idara tatu ambazo ni (Idara ya Radiolojia, Famasi na Idara ya Maabara ikijumuisha Chumba cha Kuhifadhi Maiti (Mortuary).

Kurugenzi ya Uuguzi ina idara nne ambazo ni (Idara ya Utasishaji,Huduma za Chakula, Idara ya Uuguzi na Utunzaji wa Majengo,  na Ustawi wa Jamii.

Kurugenzi ya Utumishi ina Idara mbili ambazo ni (Idara za Ajira na Mafunzo na  Idara ya Maslahi ya Watumishi). Kurugenzi ya Ufundi ina idara mbili ambazo ni (Idara ya Ufundi na Idara ya Mazingira).

Kurugenzi ya Fedha na Mipango ina idara moja ya Uhasibu ambapo Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ina Idara mbili ambazo ni  (Idara ya Kumbukumbu za Wagonjwa na Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano). Mafunzo haya yalimalizika mwishoni mwa juma.

No comments:

Post a Comment