Tuesday, April 29, 2014

Rais Dkt. Shein, akutana na Uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Kwaza wa Rais Ikulu, mjini Zanzibar


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais katika kikao cha utekelezaji Mpango kazi wa Robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja leo.
Baadhi ya maafisa wa idara mbali mbali za Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais wakiwa katika kikao cha utekelezaji Mpango kazi wa Robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja leo asubuhi,mwenyekiti wake akiwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
 
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amerejea wito wake wa kuzitaka Wizara na Idara za Serikali kutilia mkazo kazi za utafiti ili kusaidia utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Wizara na Idara hizo.
Amesema dhamira ya Serikali ya kuongeza fedha za shughuli za utafiti katika bajeti ya Serikali imelenga katika kuhakikisha kuwa Wizara na Idara za Serikali zinafanya tatifi ambazo matokeo yake yatakuwa chachu katika utekelezaji wa majukumu yao ya msingi.
Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2013/2014 katika mkutano uliofanyika Ikulu.
Kwa hiyo ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kukamilisha utafiti wa ufikiaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu ambapo matokeo yake yamekuwa msingi wa kuandaa Sera ya Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu.
Katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Mhe Rais alihimiza suala la vipaumbele vya Wizara na Idara kwenda sambamba na majukumu ya msingi ya Wizara na Idara (core functions) husika.
Kuhusu suala la msaada wa uendeshaji wa vituo vya vijana walioacha madawa ya kulevya nchini maarufu ‘Sober Houses’ Dk. Shein amehimiza ushiriki wa wadau wengi zaidi huku akiitaka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuliangalia kwa upana zaidi suala hilo ikiwemo kuandaa mpango maalum ambao utakuwa endelevu kuonesha msaada wa jamii ikiwemo Serikali kwa vituo hivyo. 
Katika maelezo yake ya awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Bi Fatma Abdulhabib Fereji alieleza kuwa  katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 Ofisi yake imeweza kukamilisha utafiti wa kubaini huduma na fursa zinazopatikana  kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na kukamilisha utayarishaji wa Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Aliongeza kuwa shughuli nyingine ambazo Ofisi yake iliendelea kuzifanya kuwa ni pamoja na kuendelea kusimamia marufuku ya mifuko ya plastiki pamoja na kuendelea kusimamia uchukuaji holela wa maliasili zisizorejesheka.
Waziri alieleza pia masuala yanayoendelea kutekelezwa na Ofisi yake ambayo yanatarajiwa kukamilishwa katika mwaka ujao wa fedha kuwa ni pamoja na Sera ya Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu, Sera ya UKIMWI, Kanuni ya Sheria ya Dawa za Kulevya, Mkakati wa Kudhibiti Taka Ngumu na Mpango wa Utekelezaji wa Mabadiliko ya Tabianchi.  
Hata hivyo Waziri alieleza pia baadhi ya changamoto ambazo Wizara yake inapambana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake zikiwemo za uingizaji uliokithiri wa bidhaa chakavu, Ugumu wa jamii kufuata taratibu za uvunaji maliasili zisizorejesheka, miundombinu isiyo rafiki kwa watu wenye ulemavu na uelewa mdogo wa jamii juu ya watu hao.
Changamoto nyingine ni ushiriki mdogo wa jamii katika mapambano dhidi ya madawa ya kulevya na unyanyapaa kwa wtu wenye virusi vya UKIMWI na watu walio katika makundi maalum.

No comments:

Post a Comment