Baadhi ya wanakijiji na Wanausalama wakifuatilia kwa Makini Kikao hicho.
*******
UONGOZI wa Kijiji cha Ikhoho Kata ya Maendeleo Wilaya ya
Mbeya unatuhumiwa kufuja fedha za michango ya maendeleo zaidi ya shilingi
milioni tatu zilizochangwa na wananchi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
Tuhuma hizo zilitolewa jana mbele ya mkutano wa hadhara
uliofanyika kijijini hapo ambao ulihudhuriwa na Polisi Tarafa,Mkaguzi wa Polisi
Galusi Ligula, pamoja na Mwenyekiti wa
Kijiji aliyeondolewa madarakani, January Mwambole na Mtendaji wa Kijiji, Wakaa
Nkembo.
Wakizungumza kwenye mkutano huo wananchi wamedai kuwa kwa kutumia
madaraka yao viongozi hao waliwatoza wanafunzi 45 wa shule ya msingi ya kijiji
hicho shilingi 525,000/- wanafunzi wakidaiwa kuvunja choo cha shule.
Walisema Wanafunzi 40 walitozwa shilingi elfu tano kila mmoja
katika ofisi ya kijiji na wanafunzi watano wakilipa shilingi elfu sitini na
tano katika Kituo cha Polisi cha Inyala ambapo waliwekwa mahabusu kabla ya
wazazi wao kulipa pesa hizo.
Waliongeza kuwa kwa kutumia madaraka yao viongozi hao walianza
kuwaandama wananchi waliokuwa wakihoji uhalali wa tozo hilo ambapo kijana mmoja
aliyefahamika kwa jina la Bahati Kitundu alifunguliwa jalada la kutishia
kufanya fujo kijijini kutokana na kuandika barua ya malalamiko kwa Mkuu wa
Wilaya ya Mbeya juu ya kero za michango mbalimbali Kijijini hapo.
Wananchi hao walisema mbali ya pesa za choo cha shule ya Msingi viongozi
hao wanatuhumiwa kutafuna michango ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ikhoho
ambazo walikusanya kutoka kwa wananchi na kutoziwasilisha sehemu husika kwa
muda mrefu na baadhi ya wananchi walikamatwa kwa kushindwa kutoa pesa hizo kwa
wakati.
Aidha katika mkutano huo Jeshi la Polisi lilitumia fursa ya kutoa
elimu kwa wananchi kutotumia mabavu katika shughuli za maendeleo na viongozi
watimize majukumu yao.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wananchi hao waliazimia kuunda
tume ya watu watano kwa ajili ya kujiridhisha na tuhuma hizo kabla ya
kuwasimamisha kazi viongozi wa Kijiji
Na Mbeya Yetu
No comments:
Post a Comment