Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo, amesema kauli hiyo ni ishara ya woga
unaojitokeza mapema, kabla ya mpambano wa kisiasa na kwamba kuingia ama
kutoka Ikulu si rahisi.
Kisumo aliyasema hayo jana wakati akiongea
na NIPASHE Jumapili, kwa njia ya simu akiwa jijini Dar es Salaam kwenye
matibabu, ambapo alisema kauli wa Membe ambaye ni Mbunge wa Mtama, ni
woga.
“Siku zote kwenye mapambano huwezi kutupa
silaha chini na kisha kukimbia, bali yapaswa kupambana hadi mwisho,”
anasema Kisumo mmoja wazee wanaoheshimika ndani ya chama hicho.
Kauli ya Membe aliitoa wakati wa chakula
cha mchana, alichowaandaliwa viongozi wa Chadema, waliokuwa katika jimbo
la Mtama kwa ajili ya utekelezaji wa Operesheni Okoa Kusini.
“Membe amekuwa mwoga mapema mno, badala ya
kupambana anatupa silaha chini na kukimbia, unapotupa silaha chini
huwezi kushinda vita iliyopo mbele yako na katika mapambano hayo huwezi
kumtabiria adui yako ushindi,” alisema.
Aliongeza, “kazi ya kuingia na kutoka Ikulu si nyepesi, ni kazi ngumu sana kwa Chadema kuingia madarakani”.
Kisumo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, alisema ni haki ya Chadema kujiimarisha kwa
kuwa CCM imeimarika tangu siku nyingi.
Hivyo, alisema hakuna ubaya kwa wao
kuingia hadi ngazi ya kitongoji ambako CCM ina mashina yake, na kwamba
hicho si kigezo cha ushindi kwao.
Alisema tatizo kubwa kwenye Chadema kuna
wanaharakati na si wanasiasa, na haiwezekani kuongoza serikali kwa kuwa
na viongozi wanaharakati.
“Hawa Chadema wanachokifanya ni kuvizia
makosa madogo madogo ya serikali na kisha kuwashawishi wananchi wawe
upande wao,” alisema.
Aliongeza, “wapo viongozi wa Chadema na
waasisi, kama Mzee Edwin Mtei na watu wengine makini ninaowafahamu ndani
ya chama hicho, sijawahi kuwasikia wakiropoka hovyo kama wanavyofanya
baadhi ya viongozi wa chama hicho.”
Alisema ikiwa hulka hiyo itandelea, kuna
hatari ya kukosa sifa ya kushika dola vinginevyo watapata shida, kwani
hakuna serikali inayoweza kwenda kwa kuendeshwa na wanaharakati.
Kisumo alisema hakatai uwepo wa upinzani na ukuwaji wake, kwani naye ni mmoja wa walioridhia mfumo wa vyama vingi kuwepo nchini.
Hata hivyo alisema inatakiwa chama ambacho
kitashinda kiwe na uwezo wa kuongoza katika hali ya amani na utulivu na
si kuingia kwenye machafuko mara baada ya uchaguzi.
Alisema ili Chadema ishike dola, ni lazima
wajitahidi kujenga safu ya uongozi wa kutawala na si kuwa na viongozi
ambao kila wakati wanahamasisha watu kuandamana, kugoma na kuvizia
makosa ya serikali iliyopo madarakani.
Alisema wanachokifanya Chadema ni sawa na
wawindaji wanaokoka moto kwa ajili ya kuchoma nyama ili hali nyama
yenyewe hawajaipata, na kwamba kazi ya kuing’oa CCM si rahisi kama
inavyofikirika.
Hata hivyo alitoa changamoto kwa watawala na kusema, “CCM inapaswa kujipanga kwa kueleza ukweli juu ya mambo mbalimbali na
kupigana vita ya kweli dhidi ya ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.”
Kisumo alisema wakati CCM ikielekea kwenye
uchaguzi wa ndani ya chama, kimejipanga kikamilifu kupata watu safi
wenye damu safi, ari mpya na nguvu mpya, ya kupambana na vyama vyote
katika kushika dola
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment