Thursday, June 12, 2014

JESHI LA POLISI LACHUNGUZA KUHUSU CHANZO CHA MOTO SOKO LA ILALA MCHIKICHINI


       Jeshi la Polisi Kanda Maalum limeanza uchunguzi  kuhusu tukio la moto mkubwa uliotokea katika soko la Mchikichini Ilala.

          Tukio hilo lilitokea ghafla majira ya saa tano za usiku ambapo bidhaa mbali mbali za wafanyabiashara ziliteketea kwa moto.  Watu walioshuhudia tukio hilo waligundua moto huo  kuwa ulianzia katikati ya soko.  Licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na kikosi cha Zimamoto na Shirika la Umeme Tanesco bado moto huo ulikuwa mkubwa sana kiasi cha kuteketeza sehemu kubwa ya soko. 

       Jitihada kubwa sana zilifanywa na Kikosi cha Zimamoto   kutoka Jiji, Bandari pamoja na kampuni Binafsi zenye magari ya Zimamoto.  Hali ilikuwa ngumu sana kulingana na bidhaa zilizokuwa zinaungua ikiwa ni pamoja na nguo, viatu, mabegi na vifaa vya plastiki ambao zilichochea moto huo kuenea kwa kasi.  

Kazi kubwa iliyofanyika ilikuwa ni kuzuia moto huo usisambae katika makazi ya watu jambo ambalo lililokuwa gumu lakini liliwezekana kupitia watendaji hapo juu.


Jeshi la Polisi lilidhibiti wizi na  upotevu wa mali na wahusika walijulishwa mara mpja wakafika na hata wale wakorofi walidhibitiwa.  Baada ya jitihada kubwa ya ziada moto huo ulizimwa majira ya saa 9.00 usiku huku ulinzi ukiimarishwa hadi asubuhi ya leo.  Aidha hakuna taarifa zozote za watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa.

          Mizigo yote iliyookolewa haikuruhusiwa kuondolewa eneo la tukio ili kusubiri uthibitisho wa wanaohusika.  Mpaka sasa haijafahamika chanzo cha moto huo na kwa kushirikiana na vikosi vyote tajwa hapo juu uchunguzi umeanza mara moja ili kujua chanzo halisi cha moto huo ikiwa ni pamoja na kutumia wataalamu wa kimaabara (Forensic Investigation).

Taarifa kamili itatolewa mara baada ya kukamilika kwa moto huo.

No comments:

Post a Comment