Monday, August 25, 2014

Mahakama yamuamuru mmiliki wa hoteli ya Snowcrest jijini Arusha kumlipa fidia mkurugenzi wa kampuni ya Grand Alliance Ltd


Mahakama kuu nchini kitengo cha biashara kanda ya Arusha imemuamuru mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa hoteli ya Snowcrest ya jijini Arusha,Wilfred Tarimo pamoja na familia yake kumlipa jumla ya $ 1.7  milioni sawa na zaidi ya sh,3 bilioni mkurugenzi wa kampuni ya Grand Alliance Ltd,James Ndika kama malipo ya awamu ya kwanza ya kununua hisa ndani ya hoteli hiyo.


Mbali na agizo hilo mahakama hiyo pia imeagiza washtakiwa wanne kati ya watano katika kesi hiyo  walipe  kiasi cha riba cha asilimia 4 ya fedha hizo  tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo na kiasi kingine cha asilimia 7 tangu kufungwa kwa shauri hilo hadi siku ya malipo.


Hukumu ya kesi hiyo ilisomwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Jaji Robert Makaramba mbele ya mahakama hiyo mara baada ya kueleza kuridhika na ushahidi uliowailishwa na upande wa mlalamikaji kupitia kwa wakili wake Melkizedek Lutema.


Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa nambari 9 ya mwaka 2012 Ndika alieleza kutapeliwa jumla ya $ 1.7 milioni  sawa na sh,3 bilioni baada ya kupatiwa hati mbili za eneo la hoteli hiyo lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba eneo la hoteli hiyo lina hati tatu.


Katika hati ya madai mlalamikaji anadai kuwa hati moja kati ya tatu ilikuwa na mkopo wenye riba wa kiasi cha sh,1.5 bilioni kupitia benki mojawapo hapa nchini na baada ya kugundulika hilo ilikwamisha biashara ya mauziano ya hoteli hiyo.


Kwa mujibu wa nakala ya hukumu iliyosainiwa na Jaji Makaramba washtakiwa watano katika kesi hiyo mshtakiwa wa kwanza ,Wilfred Tarimo,Derick Tarimo,Doreen Tarimo ambaye ni mke wa mshtakiwa wa kwanza Irene Tarimo pamoja na kampuni ya Snowcrest And Wildlife Safaris Ltd  wameamriwa kumlipa Ndika fedha hizo pamoja na kiasi cha riba hadi tarehe ya kukazia hukumu.


Mbali na agizo hilo washtakiwa wote katika kesi hiyo pia waliamriwa kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo  tangu ilipoanza kuunguruma huku wakipewa nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 30  tangu hukumu hiyo ilipotolewa.


Akihojiwa jijini Arusha wakili wa upande wa mlalamikaji,Lutema alisema kuwa wao wameridhika na hukumu hiyo na kwa sasa wanajiandaa kuwasilisha gharama za uendeshaji wa kesi hiyo tangu ilipoanza kuunguruma mnamo Januari 5 mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment