Ni
asubuhi tulivu katika fukwe za bahari ya hindi kusini mwa Tanzania
ambapo vijana wengi wamejitokeza kufanya usaili wa mashindano ya Maisha
Plus East Africa 2016. Wapo wanaoonekana kujiamini na wengine wamejawa
uoga. "Ni siku niliyoisubiri kwa hamu sana" anasema Faustine
Komba miongoni mwa washiriki kutoka Mtwara.
Safari
ya msimu wa tano wa mashindano ya Maisha Plus imeanza rasmi kwa kuanza
na usaili uliofanyika katika hotel ya NAF Beach iliyoko Mtwara.
Washiriki kutoka mikoa ya jirani nao pia walijitokeza. "Maisha Plus
kwangu ni ndoto ya muda mrefu sana, niliposikia mnakuja Mtwara nikasema
piga ua lazima nishiriki" Anasema Ismail Likando aliyesafiri kutoka
Lindi.
Maswali
mengi yalilenga kupima uelewa wa vijana kuhusu mambo mbalimbali ya
kijamii ikiwemo mtazamo wao juu ya mwenendo wa kiuchumi. Mengine
yalilenga kuwachanganya tu.
Mshiriki
Grace Pemba anaelezea changamoto mbalimbali alizokutana nazo kutokana
na kuolewa akiwa na umri mdogo, anasema hadi sasa ana watoto wawili
ambao wanaishi na baba yao. Alipoulizwa maswali zaidi Grace alijawa na
simanzi na kujikuta akitoa machozi, "Nimelia kwa sababu mmenikumbusha
nyuma nilikotokea" anasema Grace mfanyakazi wa Saloon kutoka mkoani
Mtwara.
A video posted by Maisha Plus (@maishaplus2016) on Jun 4, 2016 at 6:47am PDT
Wakati
usaili ukiendelea hali ya kujaa kwa maji baharini ilitokea na
kulazimisha timu ya Maisha Plus kubadili utaratibu wa awali wa upigaji
picha.
- Waandaaji wa mashindano ya Maisha Plus wakibadili utaratibu wa awali wa kupiga picha baada ya maji kujaa.
Muhitimu
wa shahada ya kilimo William Mbaga alibanwa kutoa ufafanuzi wa mambo
mbalimbali ikiwemo faida za kilimo cha 'greenhouse' pamoja na namna
ambavyo maziwa ya mtindi yanapatikana. William alijieleza kwa ujasiri.
Washiriki wenye fani na ujuzi mbalimbali walijitokeza wakiwemo madereva bodaboda, mafundi, waigizaji, waimbaji, wasusi n.k
- Waigizaji pia walikuwemo katika usaili wa #MaishaPlusMtwara
- Washiriki mbalimbali waliojitokeza katika usaili wa #MaishaPlusMtwara.
Mashindano
ya Maisha Plus kwa mwaka huu yanatarajia kuchukua washiriki 30 kutoka
nchi za Burundi, Rwanda, Kenya, Tanzania na Uganda ambapo mshindi
atajishindia ufadhili wa wazo la biashara lenye thamani ya Tzshs.
Milioni 30.
"Mwaka
huu washiriki wajipange sana. Maandalizi yaliyofanywa kufanikisha msimu
huu hayajawahi kutokea katika historia ya Maisha Plus. Ni kama tunaanza
moja" Alisema Masoud Kipanya, miongoni mwa majaji na waanzilishi wa
mashindano haya.
"Tumewekeza
katika teknolojia ya kisasa ili kupata picha za matukio yenye uhalisia
zaidi. Watazamaji wategemee burudani safi isiyomithirika kupitia Azam
Two." Alisema David Sevuri, miongoni mwa waanzilishi wa Maisha Plus.
Taarifa mbalimbali kuhusu mashindano haya zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya www.maishaplus.tv
No comments:
Post a Comment