Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB Thomas Samkyi
Na Tiganya Vincent, Dodoma
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeiomba Serikali kupitishia fedha zote za maendeleo katika sekta ya kilimo katika Benki hiyo ili ziweze kuwafikia walengwa kwa urahisi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB Thomas Samkyi wakati akitoa taarifa yake ya utangulizi kwenye semina ya wabunge wa Bunge la Jamhuri Muungano wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa TADB na majukumu yake.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia Benki hiyo kuwa imara ili iweze kutoa huduma zinazotarajiwa kwa wakulima ambao wengi wako vijijin .
Samkyi aliongeza kuwa kuimarika kwa Benki hiyo kutaiwezesha kutoa mikopo kwa wakulima wengi hasa wa vijijini ambao hawawezi kupata mikopo au mitaji katika Benki za biashara wala kuhimili gharama zake.
Alisema kuwa mtaji uliopo ni kidogo ambao benki hiyo haiwezi kukopesha miradi mikubwa wala mikoa mingi kwa muda mrefu kwani itakosa ukwasi katika kipindi kifupi.
Aida ,Mkurugenzi huyo alisema kuwa pamoja na uhaba wa mtaji TADB imeweza kutoa elimu kwa wakulima 45,987 ili waweze kupatiwa mikopo.
Naye Mkurugenzi wa Mipango, Utafiti na Sera wa TADB Francis Assenga Benki hiyo imeiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuweka angalau tengo la shilingi bilioni 200 katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wakati taratibu za hati fungamani zikikamilishwa.
Aliongeza kuwa Benki hiyo iliweza kuwekeza sehemu ya mtaji uliopatikana kwenye masoko ya fedha na kupata faida kidogo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB Robert Pascal alitaja maeneo 14 ya kipaumbele ya bidhaa za kilimo ambazo zinaweza kupatiwa mikopo kuwa ni kilimo cha nafaka, kilimo cha mazao ya viwanda(miwa na korosho) na ufugaji wa ng’ombe.
Maeneo mengine ni kilimo cha mboga mboga (matunda, mboga mboga na viungo) na kilimo cha mbegu za mafuta ,kilimo cha mazao ya misitu(ufugaji wa nyuki) , ufugaji wa kuku wa kienyeji na kuku wa kisasa na ufugaji wa samaki.
No comments:
Post a Comment