Wednesday, May 18, 2016

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI GEORGE MASAJU AWATAKA MAWAKILI WA SERIKALI KUWA MAKINI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju 

Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wa Serikali kuwa makini na kutoa ushauri kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu pindi wanapotoa ushauri wa kisheria kuhusu mikataba mbalimbali.
Mhe. Masaju ameitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea  na Mawakili  wa Serikali wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanayohusu uhakiki wa mikataba ya ununuzi wa umma leo Mjini Dodoma.
Alisema ni vyema wakatekeleza jukumu hilo kwa makini kwani ushauri unaotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mawakili hao ndio msimamo wa Serikali.
“Ninapenda kuwakumbusha kwamba ninyi ni watumishi wa umma na mnaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2003” alisema Mhe. Masaju na kuongeza kuwa:
“Kama walivyo watumishi wengine wa umma na kwa msingi huu, ninyi ni sehemu ya Serikali na nafasi yenu katika Serikali ni kubwa”.
Pia aliwataka wanasheria wa Serikali kujengewa uwezo kuhusu uhakiki wa mikataba na iwapo watashindwa kutekeleza wajibu huo ipasavyo watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.
Alisema kuwa kutokana na kuongezeka kwa thamani ya mikataba inayohakikiwa na wanasheria wa taasisi  ya manunuzi ni wazi kwamba kuna umuhimu wa Maafisa Sheria kupatiwa mafunzo hayo.

“Wanasheria wa Serikali wanaohakiki mikataba hii wanawajibika kuzingatia sheria zinazohusiana na mikataba husika pamoja na maadili ya Wanasheria wa Serikali katika Utumishi wa Umma kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 27 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 2005”,alisema Mhe. Masaju.

Mhe. Masaju alishauri utaratibu wa mikataba yote kuhakikiwa Dar es Salaam ubadilike kwani unasababisha ongezeko la gharama kwa taasisi za Serikali na kuchelewesha miradi.
Alifafanua kuwa Divisheni ya Mikataba iko Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee hivyo, mikataba yote ya mikoani ni lazima ipelekwe Dar es Salaam kwa ajili ya kuhakikiwa.
“Hii inasababisha wadau hasa wa kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa, Jiji na wengine walioko mikoani kusafiri na kupeleka mikataba Dar es Salaam kwa ajili ya uhakiki” alisema Mhe. Masaju.
Hivyo alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko Mikoani ili hatimaye baadhi ya Mikataba kutoka kwa wadau walioko wilayani na mikoani iwe inapelekwa katika Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko mikoani.

No comments:

Post a Comment