Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitumia salamu za
rambirambi familia ya Meya Mstaafu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt.
Didas Masaburi aliyefariki dunia jana tarehe 12 Oktoba, 2016 katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu hizo
Rais Magufuli amesema amepokea taarifa ya kifo cha Dkt. Didas
Masaburi kwa mshituko na masikitiko makubwa na kwamba anaungana na
familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki
kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.
“Poleni sana
familia ya Dkt. Didas Masaburi, najua huu ni wakati mgumu sana kwenu,
lakini niwahakikishie kuwa sote tumeguswa sana na msiba huu kwa kuwa
tumempoteza mtu muhimu, msomi mzuri, kiongozi aliyelitumikia Taifa
kwa moyo wake wote na aliyesimamia kile alichokiamini” amesema
Rais Magufuli katika salamu hizo.
Aidha, Dkt. Magufuli
amewapa pole wanachama na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao
wamempoteza Mwana CCM mwenzao pamoja na Viongozi na watumishi wa Jiji
la Dar es Salaam ambao walifanya nae kazi alipokuwa Meya wa Jiji.
Amemuombea kwa
Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
“Bwana alitoa
na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina” amemalizia Rais
Magufuli.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es
Salaam
13 Oktoba,
2016
No comments:
Post a Comment