Friday, October 21, 2016

WAZIRI MAKAMBA ASHIRIKI ZOEZI LA UPANDAJI WA MITI IRINGA


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlandege iliyo katika Manispaa ya Iringa, wakishirikiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba katika Kampeni ya Upandaji miti Shuleni hapo. 
Hali halisi ya Mto Ruaha kwa sasa, kina cha maji kimeshuka sana na kusabisha vifo kwa baadhi ya wanyama wanaotegeme Mto huo. Upungufu wa kina hicho unatokana na shughuli za kibinadamu pembeni mwa mto huo. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiwa na watendaji kutoka shamba la Umwagiliaji la Madibila ambapo inasemekana maji mengi yanapotea hivyo kuadhiri mtiririko wa maji katika mto Ruaha Mkuu.

NA Lulu Mussa, safarini Mbarali
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais mwenye dhamana ya kusimamia Muungano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba ameshiriki katika zoezi la kupanda miti katika Shule Msingi Mlandege katika Manispaa ya Iringa Mjini.

Waziri Makamba amesema kuwa suala la kupanda miti ni agenda ya kitaifa sasa na kuanzia mwakani kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari wanapo ripoti mashuleni ni lazima aje na miti ili ndipo apokelewe.

"Ndugu zangu wana Iringa, tumeazimia kupanda miti kwa wingi ili kunusuru nchi yetu kuwa jangwa, maana tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia sitini na moja (61) ya nchi yetu ni inatishia kuwa jangwa, hivyo ni wajibu wetu kunusuru hali hii" Makamba alisisitiza.

Waziri Makamba pia alitoa onyo kwa wachafuzi wa chanzo cha maji cha Mto Ruaha ikiwa ni pamoja na jamii zinazofanya shughuli za kilimo, ufyatuaji wa matofali na ujenzi pembezoni mwa mto huo kuondolewa na kwa wale watakaokaidi kushtakiwa mara moja na kuahidi kurudi tena kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo.

Kwa upande mwingine Waziri Makamba ametembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kujionea upungufu wa maji kwa kiwango kikubwa katika Mto Huo. Kaimu Mhifadhi wa Hifadhi ya Ruaha Bw. Moronda B. Moronda amebainisha kuwa upungufu huo si tu una athari kwa wanyama bali ikolojia nzima ya eneo hilo, na kubainisha kuwa kilimo cha umwagiliaji katika mashamba ya Mbarali ni chanzo kikuu cha tatizo hilo.

Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Makamba alitembelea mashamba makubwa ya Mpunga na kuagiza kufanyika kwa Ukaguzi wa mazingira kwa kuwa suala hilo ni la kisheria kwa mujibu wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Pili, Waziri Makamba ameagiza kuundwa kwa kikosi kazi kitakachojumuisha wajumbe kutoka Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Dodoma, Morogoro na wadau wa mazingira ili kubaini hasa chanzo cha tatizo hilo ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Waziri Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini, hii leo amewasili katika Mkoa wa Njombe.

No comments:

Post a Comment