Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imezinduliwa rasmi na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Charles John Tizeba katika ukumbi wa Kilimo I hivi karibuni lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea kwa urahisi na kwa bei nafuu.
Mhe Dkt. Tizeba amewataka kufanya kazi kwa umakini wa hali ya juu ili kuweza kufika lengo kuu la kuanzishwa kwa mamlaka hii. Amewataka wajumbe wa Bodi wawe wawajibikaji na wabunifu katika utendaji wa kazi zao.
Aidha Jambo kubwa ambalo alilowataka wajumbe hao kuanza nalo kulifanyia kazi ni bei ya mbolea hapa nchini ambayo ni kubwa na hivyo kupelekea wakulima wengi kushindwa kumudu kununua.
“ Suala la kushusha bei ya mbolea liwe suala la kwanza kulifanyia kazi kwa mstabali wa maendeleo ya kilimo chetu kwa wakulima wetu” alifafanunua Dkt. Tizeba.
Kushusha bei ya mbolea kutasaidia sana na kuchangia kupunguza gharama za uzalishaji wa mazao mbali mbali kwa wadau wetu, alifahamisha Mhe. Dkt. Tizeba.
Aliwataka kutazama upya sheria iliyoanzisha mamlaka hii kuona kama kuna uwezekano wa kukukabiliana na bei za mbolea ambazo zinatengenezwa kijanja kijanja mitaani ili kumuumiza mkulima mdogo.
“ Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Mbolea Tanzania ina upungufu kidogo hivyo nawaomba muitazame upya ili tuweze kufanya marekebisho madogo katika sheria hii” aliongeza Dkt. Tizeba.
Pia Dkt. Tizeba aliwatahadharisha wajumbe kuwa wanafanyakazi miongoni mwa watu matajiri na wanyonge sana, hivyo wajihadhari kuingia katika mtego wa vivutio vya rushwa.
“Wajumbe acheni tabia ya kutaka “kuonwa” na matajiri kwani mnaweza kupoteza uadilifu katika utekelezaji kazi zenu na kujikuta mnajiingiza katika kashfa za kukosa uaminifu” alisisitiza Dkt. Tizeba.
Mhe. Charlse Tizeba pamoja na Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Mshindo Msolla wa pili kutoka kushoto.
Kutokana na hali hiyo alienda mbali zaidi kwa kuwapa pole Wajumbe wa Bodi kwa kuwa watafanyakazi katika mazingira magumu kwani wako midomoni mwa watu wenye fedha.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya kilimo hapa nchini yako mikononi mwao kwa kiasi kikubwa kwani wao ndio chanzo cha maendeleo ya kilimo kwa wakulima wetu waliowengi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Mshindo Msolla amemhakikishia Mhe. Dkt. Tizeba kuwa watafanyakazi kwa uwezo wao wote ili kufikia lengo lao.
“ Hatuwezi kukuangusha hata kidogo tutafanya kazi kwa bidii na uzalendo wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa letu “ aliahidi Dkt. Msolla.
Wajumbe wa Bodi hiyo ni pamoja na Dkt. Mshindo Msolla ambaye atakuwa ni Mwenyekiti na anatoka Taasisi inayojishughulisha na Biahshara ya Mbolea ( AFAP), Dkt. Ernest Marwa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Dkt. Matilda Kulumuna kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mlingano cha mkoani Tanga na Dkt. Mwijarubi Nyaruba ambaye anatokea Tume ya Mionzi Tanzania ( Tanzania Atomic Energy Commission).
Wajumbe wengine ni Bw. Farank Mushi ambaye anatokea Umoja wa Wauzaji wa Mbolea Tanzania ( TANADA), Bw. Arnold Kisinga mjumbe kutoka NEMC na kutoka Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) ni Bw. Nickonia Mwambene, Hawa Kihwele kutoka MVIWATA na kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi ni Bw. Canuth Komba na Bw. Sospeter Mtemi.
No comments:
Post a Comment