Tuesday, November 29, 2016

MKAPA AONYA-MAAGIZO, AMRI ZA VIONGOZI ZITAUA ELIMU.

Wakati Serikali ikiendelea na mkakati wa kubadilisha mfumo wa elimu, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa amesema maagizo na amri za viongozi zinazotolewa bila ya kuwa na majadiliano, zitaitumbukiza shimoni elimu ya Tanzania.

Mbali na hilo, Mkapa, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa vyuo vikuu nchini, ni lazima iendane na ubora wa miundombinu pamoja na bajeti ya Serikali badala ya kujaza wanafunzi wakati hakuna fedha za kutosha na hivyo kuwa mzigo.

Mkapa alitoa kauli hiyo jana wakati wa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambako alikuwa mgeni rasmi.

Mkuu huyo wa Udom alisema maagizo peke yake, hayaondoi matatizo ambayo yamejitokeza katika siku za hivi karibuni.

Alisema njia bora ya kuboresha elimu nchini ni kwa wadau kukutana katika meza ya mazungumzo ili wajadili changamoto zinazowakabili na kueleza nini kinatakiwa.
“Amini nawaambia, maagizo peke yake hayaondoi matatizo tuliyonayo ndani ya elimu, bali niwaombe wadau pamoja na wizara husika kuwa wakae meza ya mazungumzo ili wazijadili changamoto hizo,” alisema Mkapa.

Alisema kama maagizo yataendelea bila ya kuwepo na majadiliano elimu ya Tanzania itakuwa imewekwa rehani na kwamba katika kipindi cha miaka michache nchi haitakuwa kwenye ubora wa elimu kama ambavyo wengi wanadhania.

Alisema hayo wakati kukiwa na malalamiko ya wanafunzi yanayotokana na kuondolewa kwenye orodha ya wanaotakiwa kupata mikopo, huku wanafunzi waliokuwa wakisoma kozi maalumu ya ualimu wa sayansi wakiondolewa na vyuo binafsi vya elimu ya juu vikilalamikia kutopangiwa wanafunzi.

Pia serikali ilitangaza kubadilisha upangaji wa madaraja ya matokeo ya elimu ya sekondari kutoka mfumo wa kupanga kwa kutumia GPA na kurudisha mfumo wa divisheni.

Kwa kawaida mgeni rasmi kwenye mahafali ya vyuo vya elimu ya juu huwa hahutubii, lakini Udoma ilimuomba aseme machache baada ya kutunuku wahitimu.
“Katika machache mliyotaka niseme ni pamoja na kuwataka Serikali waache kutegemea wawekezaji, maana vyuo vyenyewe vimewekezwa. Bado nasisitiza kuwa wafanye mikutano ya pamoja na waitane kwa haraka wazungumze bila ya kutegeana,” alisema.
Awali mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Gaudensia Kabaka alimweleza Mkapa kuwa Udom inakabiliwa na kazi kubwa mbili ambazo ni kutopelekewa fedha kutoka Bodi ya Mikopo pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi waliotoka Chuo Kikuu cha St Joseph ambao wamefanya chuo kipate shida ya namna bora ya kuwasaidia kwani masomo waliyokuwa wanasoma hayaeleweki.

Mwezi Februari, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ilifuta hati ya usajili ya kampasi mbili za Chuo Kikuu cha St Joseph za Sayansi ya Kilimo na Teknolojia na Chuo cha Tehama na kusema wanafunzi 2,046 waliokuwa wakichukua shahada na stashahada wangehamishiwa vyuo vingine.

Kuhusu changamoto ya fedha, Mkapa alisema Bodi ya Mikopo imewakwamisha kwa kiasi kikubwa kutokana na kutopeleka Sh6.5 bilioni ambazo ni ada ya wanafunzi katika mwaka wa masomo 2015/16.

Mwenyekiti huyo alisema deni hilo limeharibu taswira nzima ya Udom na kuwafanya wadau washindwe kuwaamini katika utoaji wa huduma mbalimbali, kama kushindwa kuendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi.

Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Kikula alisema kulikuwa na jumla ya wahitimu 4,839 wa kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili, na shahada ya uzamivu.

*Chanzo* : www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment