Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (katikati aliyevaa miwani), akiangalia ukuta uliojengwa na mtu aliyetumia nyaraka za Kikoloni zilizofutwa kufuatia Tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mwaka 1964, mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964. Kulia kwa Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Issa Juma akimpatia maelezo ya jinsi Serikali ya wilaya hiyo, ilivyochukua hatua dhidi ya mtu huyo. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi Seif akizungumza na Wagonjwa na Wafanyakazi wa Kituo cha Afya cha Kitope akiwahamasisha kushiriki katika uchunguzi wa Afya zao utakaotolewa na Madaktari Mabingwa kutoka nchini India katika Kituo cha Afya cha Mahonda.
Balozi Seif akipokea maelezo kutoka kwa Muuguzi, Stara Ali Moh’d wa Kituo cha Afya cha Kitope (hayupo pichani), kuhusu utatuzi wa changamoto zilizokuwa zikikikabili kituo hicho ikiwa ni pamoja na huduma za maji safi na salama.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/11/2016.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kwamba uamuzi uliotolewa na Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “B” kufuatia Mtu aliyejenga ukuta kwa nia ya kuzuia eneo la Ardhi katika Kijiji cha Kazole wa kumtaka avunje Ukuta huo hadi ifikapo Tarehe 30 Novemba mwaka huu uko pale pale.
Alisema kitendo cha Mtu huyo aliyetambuliwa kwa Jina moja la Bibi Fadia cha kudai umiliki wa eneo hilo kwa kutumia nyaraka za zamani za Utawala wa Kikoloni zinakwenda kinyume na Tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kufuta nyaraka zote za kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua ukuta uliozunguushwa katika maeneo mawili tofauti zikiwemo nyumba za baadhi ya Wananchi pembezoni mwa Barabara katika kijiji cha Kazole Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Uanguja.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kukabiliana na vitendo vya ghilba vinavyoonekana kuibuka katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ambapo baadhi ya watu wanajitokeza kudai maeneo ya ardhi kwa kutumia hati na nyaraka zilizofutwa rasmi na Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kaskazini “B” kuhakikisha kwamba agizo lililompa muhusika huyo la kuvunja kuta zake analitekeleza kabla ya Serikali kuchukuwa mkondo wake wa Sheria ikiwemo kuvunja kuta hizo kazi ambayo muhusika huyo atalazimika kulipia gharama hizo.
Balozi Seif aliwaonya baadhi ya Wananchi wanaopewa maeneo ya Kilimo au ujenzi wa Makaazi kupitia Mamlaka zinazohusika na Ardhi kuacha tabia ya kurubuniwa na Watu wanaotumia fedha kuwahadaa katika kutaka kuwapokonya kijanja maeneo yao.
Alisema Serikali Kuu haitasita kuwafutia hati na nyaraka Wananchi hao wakionekana kwenda kinyume na makubaliano waliyopewa na badala yake watapewa wale watakaohitaji maeneo hayo kwa kuyatumia kwa lengo lililokusidiwa.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Issa Juma alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Serikali ya Wilaya hiyo kupitia Halmashauri yake ilimpa barua ya kusitisha ujenzi wowote mtu huyo baada ya kukosa vielelezo vinavyotambulika na Wizara inayohusika na masuala ya Ardhi.
Nd. Issa alisema Uongozi huo wa Serikali ya Wilaya ulilazimika kutoa agizo la kumtaka avunje kuta zake kabla ya Tarehe 30 Novemba 2016 baada ya kubaini kukiuka amri aliyopewa na Serikali ya Wilaya.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba wananchi wa Wilaya ya Kaskazini B na vitongoji vyake kujitokeza kwa wingi ifikapo Tarehe 3 na 4 Mwezi Disemba kuangalia afya zao katika Kituo cha Afya Mahonda.
Akizungumza na wagonjwa pamoja na watendaji wa Kituo cha Afya Kitope Balozi Seif alisema ujio wa Wataalamu Mabingwa kutoka Nchini India utatoa fura kwa wananchi kupata muda wa kuchunguza afya zao yakihusishwa maradhi ya macho, Kisukari pamoja na sindikizo la damu { Blood Pressure }.
Alisema wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo katika uchunguzi huo hasa yale matatizo ya macho wataandaliwa utaratibu maalum wa kupatiwa tiba katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Kambi hiyo awali ilikuwa imepangwa kufanyika katika Kituo cha Afya Kitope lakini kutokana na sababu za kimsingi Wataalamu wa Sekta ya Afya wamependekeza kambi hiyo kufunguliwa katika Kituo cha Afya cha Mahonda kwa vile kimebahatika kuwa na vifaa vingi vya uchunguzi vitakavyorahisisha kazi zao.
No comments:
Post a Comment