Tuesday, November 29, 2016

SERIKALI YAPOKEA MSAADA WA KOMPYUTA ZENYE THAMANI YA SH. MILIONI 500

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Bayport Tanzania Bw. John Mbaga (kushoto) wakati wa hafla yakupokea msaada wa kompyuta 205 zilizotolewa na Bayport Tanzania leo iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza wakati wa hafla yakupokea msaada wa kompyuta 205 zilizotolewa na kampuni ya Bayport Tanzania leo iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi. 
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa hafla yakupokea msaada wa kompyuta 205 zilizotolewa na kampuni ya Bayport Tanzania leo iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akipokea msaada wa kompyuta 205 zilizotolewa na Kampuni ya Bayport Tanzania leo, wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta hizo iliyofanyika Ofisi ya Rais-Utumishi. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akiwa katika picha ya moja na wajumbe  kutoka  Kampuni ya Bayport Tanzania na maofisa wa Ofisi yake mara baada ya kupokea msaada wa kompyuta 205 .Kulia kwake ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Utumishi Dkt. Laurean Ndumbaro.

Na May Simba-Maelezo
TAASISI ya kifedha ya Bayport imetoa msaada wa kompyuta 205 zenye thamani ya Sh. Milioni 500 kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za Serikali.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa kompyuta hizo zitasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za Serikali.

Amesema kuwa kati ya komputya hizo, komputya 125 zitabaki kwenye Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na zilizobaki 80 zitagawanywa kulingana na mahitaji ya Ofisi zake nyingine.

Waziri Kairuki ameongeza kuwa kompyuta hizo pia zinatarajiwa kutumika katika shughuli za usimamizi wa taarifa za watumishi na mishahara.

“Natoa wito kwa Taasisi binafsi nchini kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii ili kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi” Alisema Waziri Kairuki.

Aidha Waziri Kairuki ameiomba Taasisi ya kifedha Bayport kupunguza riba katika mikopo wanayoitoa, kuongeza kiwango cha fedha wanazokopesha watumishi wa umma ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa ni vema ikaongeza wigo wa utoaji wa mikopo ikiwemo mikopo ya viwanja, elimu na biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bayport John Mbaga alisema msaada wa Kompyuta hizo zinatokana na kiu yao kubwa ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa ajili ya kufanikisha huduma bora kwa Watanzania.

“Sisi jukumu letu ni kushirikiana na Serikali sambamba na kujitolea kwenye jamii kwa kusaidia mambo mbalimbali kwa ajili ya kukwamua wateja wetu kwa ujumla kwa kupitia sekta ya mikopo”.Alisema Mbaga.

Makabidhiano ya Kompyuta hizi ni sehemu ya kusheherekea miaka 10 ya huduma za Bayport ilipoanzishwa mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment