Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Serikali Mtandao, Michael Moshiro, akizungumza. Kushoto ni Meneja wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano e-GA, Bi. Suzan Mshakangoto.
Na Beatrice Lyimo, Maelezo
10/11/2016
Dar es Salaam.
SERIKALI kupitia Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) imetoa wito kwa taasisi za Sekta binafsi wanaojishughulisha na utoaji wa huduma za TEHAMA na ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kujenga uelewa wa viwango na miongozo ya TEHAMA ili kuisaidia Serikali.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Serikali Mtandao, Michael Moshiro wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliolenga kujenga uwezo kwa waandishi hao kuhusu utekelezaji wa Serikali mtandao nchini na ufafanuzi wa miongozo na viwango vya TEHAMA Serikalini.
“Nitoe rai kwa sekta binafsi hasa kwa wale wanaojihusisha na utoaji wa huduma za TEHAMA na ujenzi wa mifumo ya TEHAMA ni vema wawe na uelewa wa viwango na miongozo ili kuweza kuisaidia Serikali” alifafanua Moshiro
Alisema Serikali imeanza kutumia miongozo na viwango ya TEHAMA hivyo ni muhimu kwa wataalamu wa TEHAMA wanaotaka kufanya kazi na Serikali kuanza kujenga mifumo inayozingatia viwango hivyo.
Aidha, alisema kuwa miongozo na viwango ya TEHAMA Serikalini ina lengo la kusaidia Serikali katika kutumia TEHAMA kwa usahihi katika kuhakikisha utendaji kazi wa Serikali unaboreshwa na utoaji wa huduma kwa wananchi unarahisishwa.
Aidha Moshiro alisema kumekuwa na faida mbalimbali za uwepo wa matumizi ya miongozo na viwango hivyo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya TEHAMA ikiwemo kuwezesha mifumo kujengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya taasisi husika na Serikali kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Moshiro alisema Serikali pia imefanya jitihada za kuhakikisha uwepo wa Sera, sheria, miongozo na mikakati madhubuti inayotumika katika utekelezaji wa jitihada za Serikali mtandao.
No comments:
Post a Comment