Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi YA JKCI, Profesa Mohamed Janabi
Na Anna Nkinda - JKCI
21/11/2016
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa kiasi cha shilingi milioni 580 fedha ambazo Serikali ingezitumia kwa kuwapeleka wagonjwa wa moyo 20 nchini India kwa ajili ya matibabu ambapo kwa kila mgonjwa angegharamiwa kiasi cha shilingi milioni 29.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi alipokuwa akielezea kuhusu upasuaji kwa wagonjwa wa moyo wanaoufanya hivi sasa kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Moyo kutoka Taasisi ya Open Heart International (OHI) ya Nchini Australia.
Prof. Janabi aliongeza kuwa upasuaji huo wa wagonjwa unaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa wataalamu wa ndani wakiwemo madaktari, wauguzi, wagavi na mafundi wanaohusika na utengenezaji wa mashine za kimatibabu.
“Idadi ya wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji ambao utachukuwa muda wa siku sita ni 20 kati ya hao watoto ni 15 na watu wazima ni watano”.
“Tunafanya upasuaji kwa wagonjwa watatu kwa siku hadi sasa jumla ya wagonjwa nane wameshafanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri kati ya hao watu wazima watatu na watoto watano”, alisema Prof. Janabi.
Alizitaja gharama wanazolipa wagonjwa hao ni shilingi laki tano kwa ajili ya vipimo vya maabara hii ni kwa wagonjwa wenye uwezo wa kulipia, kwa wagonjwa wasio na uwezo wanalipiwa na Serikali, Rotary Club Dar es Salaam na Bahari Beach na BAPS Charity na wagonjwa ambao ni wanachama wa Bima ya Afya wanalipiwa na bima zao.
Prof. Janabi alisema, “Wagonjwa wanaotumia kadi za Bima ya Afya ni wachache, nawashauri wananchi wajiunge na Bima ya Afya kwani gharama za matibabu ni kubwa na tunakoelekea watu hawataweza kulipa na sisi kama Taasisi hatuwezi kufanya upasuaji bure kwani tunahitaji kununua vifaa tiba ili tuweze kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa wetu”.
Alizitaja changamoto wanazikabiliana nazo katika zoezi hilo la upasuaji kuwa ni pamoja na damu kwani wanatumia damu chupa sita hadi nane kwa mgonjwa mmoja hii inatokana na wagonjwa kutokuwa na damu ya kutosha.
Tangu mwaka 2015 Taasisi hiyo imekuwa ikifanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Taasisi za kimataifa zikiwemo za OHI, Okoa Moyo wa Mtoto (Save Child Heart –SACH) na Mending Kids (MKI) ya nchini Marekani na madaktari kutoka nchi hizo wamekuwa wakija na vifaa tiba na kijigharamia nauli.
No comments:
Post a Comment