Wednesday, February 15, 2017

SERIKALI YA JAPAN YAISAIDIA TANZANIA DOLA 80,234 KUENDELEZA MCHEZO WA BASEBALL

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mhe. Nape Nnauye (aliyesimama mbele) akiongea na Wageni waalikwa pamoja na Waandishi wa habari wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Benedict Liwenga-WHUSM)
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Masaharu Yoshida (aliyesimama mbele kulia) akiongea na Wageni waalikwa pamoja na Waandishi wa habari wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na Wachezaji wa mchezo wa Baseball mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na Wachezaji wa mchezo wa Baseball pamoja na Viongozi wa Michezo pamoja na viongozi toka Ubalozi wa Japan mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam. 
Mwenyekiti wa Chama cha Baseball Tanzania (TaBSA), Dkt. Ahmed Makata (aliyekaa kushoto mbele) akisaini Mkataba wa Ujenzi wa Uwanja wa Baseball, kulia ni Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Masaharu Yoshida. Wanaoshuhudia nyuma ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye pamoja na Mjumbe toka Japan.

Na Mwandishi wetu
SERIKALI ya Tanzania na Japan zimetiliana saini Mkataba wa Dola za Kimarekani 80,234 sawa na shilingi za Kitanzania milioni 170 zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha mchezo wa Baseball.
Hafla ya Utiaji saini wa Mkataba huo umefanywa leo na Balozi wa Japan nchini Mhe. Masaharu Yoshida pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Baseball Tanzania (TaBSA), Dkt. Ahmed Makata  huku ukishuhudiwa na mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye.

Akiongea na Waandishi wa Habari pamoja na wageni waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Nape amesema kwamba, Serikali ya Japan imekua na uhusiano mzuri ambapo nchi hiyo imekuwa ikiisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya michezo.
Aidha, Waziri Nape amemuagiza Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw.Yusuph Singo kuhakikisha kuwa mchezo wa baseball unasambaa mashuleni ili kuweza kuvumbua vipaji zaidi kwa vijana.
Ameongeza kuwa, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya TAMISEMI imetenga jumla ya shule 55 za sekondari kwa ajili ya michezo mbalimbali nchini.
“Naishukuru Serikali ya Japan kwa msaada mliotupatia tutahakikisha kwamba mchezo huu wa baseball unasambaa mashuleni na kupendwa zaidi na vijana wetu”, alisema Mhe. Nape.
Kwa upande wake Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Masaharu Yoshida amesema kwamba, msaada wa fedha hizo utasaidia ujenzi wa kiwanja cha mchezo wa baseball katika shule ya Sekondari ya Azania iliyopo Jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa, mradi huo umekua ni alama ya Japan kwa umoja wao yaani Serikali ya Japan, Wakala wa Mahusiano ya Kimataifa wa Japan (JICA), Makampuni binafsi ya Japan na Chama cha Marafiki wa Baseball Afrika (AFAB) katika jitihada zao za pamoja za kupanda mbegu za mchezo huo Barani Afrika ikiwemo Tanzania.
“Nina imani kuwa, chini ya nidhamu njema ya Shule ya Sekondari ya Azania na Chama cha Baseball Tanzania, kiwanja hiki kitatunzwa ili kiweze kuwa urithi wa Taifa na vizazi vijavyo”, alisema Balozi Yoshida.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Baseball Tanzania (TaBSA), Dkt. Ahmed Makata ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mchango wake mkubwa inaoutoa katika kuuendeleza mchezo huo, na kwa upande mwingine ameishukuru Serikali ya Japan kwa msaada wa ujenzi wa kiwanja cha baseball ambacho kinatarajiwa kujengwa hapa nchini.
Mchezo wa Baseball Tanzania ulianzishwa na Wataalam wa Wakala wa Mahusiano ya Kimataifa wa Japan (JICA) ambapo Wakala huo umekuwa mstari wa mbele katika kuuendeleza mchezo huo kwa kusaidia katika masuala ya mafunzo pamoja na vifaa na mapema mwezi Machi mwaka huu, JICA inatarajia kuleta Mtaalam kutoka Japan ambaye atasaidia kutoa mafunzo juu ya mchezo huo kupitia TaBSA, na kupitia JICA, TaBSA imepata seti 25 za vifaa vya mchezo huo.

No comments:

Post a Comment