SERIKALI YASISITIZA UHURU WA MIHIMILI, MIKAKATI YA
KUKABILIANA NA MAJANGA YA ASILI
Dodoma, Alhamisi, 2 Februari, 2017:
Serikali imetoa
ufafanzi kuhusu masuala mbalimbali kuhusu utawala wa Sheria na kuainisha mikakati
yake katika kuzuia au kupunguza athari za matetemeko ya ardhi nchini. Ufafanuzi
huo umetolewa mjini hapa leo.
Serikali Kutoingilia Mihimili ya Dola
Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu mgawanyo wa mihimili
mitatu ya dola nchini. Waziri Mkuu alikuwa akifafanua kuhusu malalamiko kuwa
baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kesi zao zinachukua muda mrefu.
Aidha, Waziri
Mkuu amekanusha vikali madai kuwa Serikali inakusudia au imetangaza kufuta
vyama vya siasa hasa vya upinzani nchini madai yaliyotolewa na Kiongozi wa
Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe.
Mkakati
Kuzuia Majanga Ya Asili
Akijibu hoja
kuhusu mikakati ya kupambana na athari za majanga ya asili, Naibu Waziri, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde, amesema Serikali tayari
inao mkakati wa kitaifa wa kupambana na majanga ya asili yakiwemo matetemeko.
Aidha,
Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo imeainisha aina
mbalimbali za maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na majukumu ya kila mdau
katika kushughulikia maafa. Aliongeza kuwa, Serikali pia imeandaa Mwongozo wa
Taifa wa Kukabiliana na Maafa ambao unaelekeza Taasisi kiongozi na wajibu wao
wakati wa kukabiliana na majanga.
Liganga, Mchuchuma Kuzalisha Megawati 350
Serikali
imesema kuwa, miradi unganishi ya Mchuchuma na Liganga itakayotekelezwa kati ya
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Group (SHG)
Limited ya China kupitia ubia wa pamoja wa Tanzania China International Mineral
Resources Limited (TCIMRL) itazalisha zaidi ya ajira 33,000 na kuipatia nchi
umeme wa megawati 350.
Akitoa
ufafanuzi huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema
kuwa kampuni hiyo imeshapewa leseni na
vibali vingine muhimu na sasa inakamilisha ulipaji wa fidia ili kuanza kazi.
“Miradi hiyo unganishi itawezesha kuchimbwa makaa ya mawe kiasi cha tani
milioni (3) na chuma ghafi tani milioni 2.9 kwa mwaka,” alisema.
Usalama wa Raia Mipakani
Serikali
kupitia vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo ya mipaka inachukua hatua za
pamoja na vyombo vya nchi jirani kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao
katika maeneo hayo.
Akijibu hoja
kuhusu suala la usalama wa raia wanaoishi pembezoni mwa mipaka ya Tanzania,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amefafanua kuwa
operesheni za pamoja zinafanyika katika mipaka ya nchi na vikao vya ujirani
mwema ili kuhakikisha usalama. Wananchi wameombwa kutoa taarifa wanapowaona
wageni wasioeleweka katika maeneo yao ili kuimarisha usalama.
Wanahabari
Waendeleze Kiswahili
Serikali
imewapa changamoto wanahabari nchini kuwa chachu ya kuendeleza lugha ya
Kiswahili. Wakijibu maswali mbalimbali ya wabunge kuhusu matumizi ya Kiswahili
fasaha katika vyombo vya habari, Waziri na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, wameliambia Bunge kuwa, ni vyema sasa hata wamiliki wa vyombo
vya habari wakaanza kuzingatia ufaulu kwa somo la Kiswahili kabla ya kuwaajiri
waandishi.
Kwa upande
wake Waziri Nape akitoa majibu ya nyongeza, alisema kuenziwa kwa Kiswahili
nchini kumeipa Tanzania hadhi ya kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za
Afrika zinazojihusisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment