Wednesday, July 31, 2013

MFUKO WA PENSHENI KWA WATUMISHI WA UMMA (PSPF) wajipambanua


Meneja Mawasiliano,Masoko na Uenezi kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) Bi.Constantina Martin(kulia) akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam kuhusu Mpango Mpya wa uchangiaji wa hiari mahususi kwa ajili ya kuwapatia wananchi wasio wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii fursa ya kujiunga na mfuko huo, kushoto ni Mkurugenzi wa Uwekezaji, mipango na Utafiti Bw. Gabriel Silayo.
Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mipango na Utafiti kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) Bw. Gabriel Silayo(kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo yaliyofikiwa na mfuko huo tangu kuanzishwa kwake kulia ni Meneja Mawasiliano,Masoko na Uenezi kutoka Mfuko huo Bi.Constantina Martin. (Picha zote na Frank Mvungi, Maelezo)

1.0    UTANGULIZI
PSPF ni Taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa Sheria Namba 2 ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma ya mwaka 1999 (The Public Service Retirement Benefits Act No.2 of 1999) sura ya 371.
Hapo awali Mfuko huu ulikuwa unahudumia watumishi wa Serikali Kuu na Wakala wa Serikali tu. Hata hivyo, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Msimamizi na Mdhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (Sheria Na.8 ya mwaka 2008); fursa zaidi zimefunguliwa ambapo sasa Mfuko wa PSPF unaweza kusajili wanachama kutoka sekta zote iwe sekta binafsi, sekta rasmi na isiyo rasmi.  Aidha  mabadiliko haya yameleta uhuru kwa mtumishi kuchagua Mfuko autakao.
Kutokana na hili PSPF inapenda kuwakaribisha wote na inatoa taarifa rasmi kwamba sasa kila Mtanzania aliyepo ndani au nje ya nchi anaweza kuwa mwanachama wa PSPF! Ili kuweza kuwahudumia Watanzania wote haswa waliopo katika sekta isiyo rasmi PSPF imeanzisha Mpango wa Uchangiaji wa Hiari (PSPF Supplimentary Scheme) maarufu kama PSS.
Mpango huu ulizinduliwa rasmi tarehe 07 Machi 2013 wakati wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wadau wa PSPF, hadi kufikia tarehe 25/07/2013 mpango huu una wanachama 730 na makusanyo ya kiasi cha shilingi milioni 135.83.
2.0    MPANGO WA UCHANGIAJI WA HIARI (PSPF SUPPLIMENTARY SCHEME- PSS)
Mpango huu wa hiari ni mahsusi kwa ajili ya kuwapatia huduma ya hifadhi ya jamii wale wote ambao awali kutokana na matakwa ya kisheria hawakuweza kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.  
Vile vile mpango huu ni fursa nzuri ya kujiwekea akiba ya ziada wanachama ambao tayari wamo katika Mifuko mbalimbali ya Hifadhi ya Jamii.
Uanachama katika mpango huu uko wazi kwa kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea. 
Kiasi cha mchango kwa mwezi ni shilingi 10,000/= kiwango ambacho wengi wanaweza kukimudu kwa mwezi na hakuna kiwango cha juu. 
Michango inaweza kuwasilishwa kwa siku, wiki, mwezi na hata kwa msimu kutegemeana na upatikanaji wa kipato cha ziada. Michango hii huwekewa faida kila baada ya miezi sita.
Michango inaweza kuwasilishwa kupitia akaunti ya benki, au kupitia Wakala wa malipo wa M-Pesa, Tigo-Pesa na Airtel money. 
Mwanachama atajaza fomu na kupewa kitambulisho na nambari ya uanachama.
Mafao yatolewayo katika mpango huu wa hiari ni kama yafuatavyo:
·         Fao la Elimu, 
·         Fao la Ujasiriamali,
·         Fao la Uzeeni,
·         Fao la Ugonjwa,
·         Fao la Kifo.
Pia mwanachama anapolazimika kuchukua michango yake yote na faida kutokana na sababu zozote zile, anaweza tena kuanza kuchangia upya bila masharti yoyote.
Taarifa hii imetolewa na:
Kaimu Mkurugenzi Mkuu
Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF)
Golden Jubilee Towers, Front Tower,
Ghorofa ya 6 -13, Mtaa wa Ohio/Kibo,

No comments:

Post a Comment