Tuesday, May 2, 2017

SERIKALI YA ZANZIBAR YAONGEZA MSHAHARA KWA ASILIMIA MIA MOJA

NA MWANA HAMAD, ZANZIBAR.

SERIKALIi ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea na utaratibu wake wa kuzilinda haki zote za wafanyakazi  na kuimarisha maslahi yao hatua kwa hatua ili waweze kumudu hali ya maisha pamoja na kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwenye sektka mbali mbali.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa msimamo huo  leo huko katika viwanja vya Mpira Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi ambayo kilele chake hufanyika kila tarehe 01. Mei ya kila mwaka duniani kote.

Katika hotuba yake  Dk. Shein amesema kutokana na kujali kazi na kuufahamu umuhimu wa wafanyakazi pamoja na kuufahamu wajibu wake akiwa Rais wa Zanzibar amechukua hatua ya kupandisha mishahara na posho mbali mbali kadri hali ya uchumi na ukuaji wa mapato inavyoruhusu.

Aidha, ameeleza kwamba  wakati wa Kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2015, aliahidi tena kuwea Serikali atakayoiongoza katika kipindi cha pili mwaka 2015 na 2020 itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa sekta ya Umma kwa aslimia 100 kutoka TZS. 150,000 hadi  TZS 300,000.

Kwa maelezo yake aliahidi kuwa mabadiliko hayo ya mshahara yataanza mwishoni mwa mwezi wa April, 2017 na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha pamoja na Serikali yake kwa kutekeelza ahadi hiyo ambapo kuanzia mwezi uliopita wafanyakazi wote wa Sekta ya Umma wameanza kufaidika na nyongeza hiyo ya mishahara.

Amesema  ongezeko hilo limetekelezwa kwa wafanyakazi na maafisa wa ngazi mbali mbali kwa viwango tofauti vilivyowekwa na Taasisi zinazohusika kulingana na kwiango cha mshahara anachokipata mfanyakazi.

 Dk. Shein pia, aliahidi kuwa Serikali itazishughulikia  changamoto chache kama zitakuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi zilizojitokeza kulingana na utaratibu uliowekwa na kuwahakikishia wafanyakazi kuwa zitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Pia, Dk. Shein amegusia kupunguzwa kwa kiwango cha kodi ya mapato katika mishahara kutoka asilimia 13 hadi 9 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, hatua hizo zote zimechukuliwa kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ufanisi katika kazi.

Ametoa  wito kwa wafanyabiashara na watoaji huduma ambali mbali, kuacha mtindo wa kuongeza bei za bidhaa na huduma bila ya sababu za msingi kwani matokeo yake na wao wanaweza kuathirika na wasije wakawalaumu wananchi na Serikali yao.

Kwa upande wa wafanyakazi katika sekta binabsi, Dk. Shein aliwajuulisha kuwa taratibu za kisheria zinaendelea ili kutangaza na kulipwa kwa kima kipya cha mishahara katika sekta hiyo.

Hata hivyo hakuacha nyuma  wafanyakazi wa majumbani, Dk. Shein alitoa nasaha zake kwa waajiri wa wafanayakzi hao kujenga utamaduni wa kuwathamini, kuwatambua rasmi, kuwapatia stahikli zao, kuwawekea mazingira ya kazi yanayostahiki na wao wapate fursa ya kujadiliana na waajiri wao kama zilivyo kada nyengine.

Nae Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico ameeleza kuwa  juhudi zinazoendelea katika kulitafutia ufumbuzi suala la kima kipya cha mishahara kwa sekta binafsi huku akitumia fursa hiyo kupongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake za kuwaenzi wafanyakazi.

Katibu Mkuu Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar, Khamis Mwinyi Mohammed amemsifu Dk. Shein kwa kutekeleza ahadi yake ya kupandisha mishahara kwa kima cha chini sambamba na kupongeza Serikali chini ya uongozi wake kwa kudumisha amani na utulivu na kueleza baadhi ya mafanikio yaliopatikana katika uongozi wa Dk. Shein.

Mapema Dk. Shein amepongeza maandamano ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma pamoja na Sekta binafsi na kabla ya hotuba yake alitoa zawadi kwa wafanyakazi bora 16 kwa niaba ya wenzao 100 kutoka sekta ya Umma.

 Sherehe hizo ambazo viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, Sekta binafsi na Serikali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, Dk. Shein aliongeza kuwa katika nyakati mbali mbali za uongozi wake katika kipindi cha kwanza cha uongozi wake alipandisha mishahara mara tatu, mwaka 2011, 2013 na mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment